Serikali ya Russia imeonya kuhusu matokeo mabaya ya kuanzisha chokochoko yoyote dhidi ya Iran.

Sergei Lavrov Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia kwa mara nyingine ameionya Marekani kuhusu matokeo mabaya ya chokochoko yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran. Lavrov alisema Jumatatu jioni, Februari 9, katika Jukwaa la 15 la Asia Magharibi la Klabu ya Mazungumzo ya Kimataifa ya Valdai (The Valdai Discussion Club), kwamba chaguo la kijeshi dhidi ya Iran halidhamini usalama wa nchi yoyote. Alisema: Chaguo la kijeshi dhidi ya Iran litazidisha matatizo yaliyopo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisisitiza kwamba msimamo wa Moscow umejengeka juu ya msingi wa utatuzi kwa njia za amani.

Siku ya Jumatatu, Lavrov pia alitangaza katika katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr bin Hamad Al Busaidi kwamba, Moscow na Muuscat zinaamini kwamba mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu suala la nyuklia yanapaswa kuendelea ili kufikiwe makubaliano “yanayokubalika kwa pande zote” na kudhamini usalama wa kikanda.

Katika wiki za hivi karibuni, hasa kutokana na ongezeko la kupelekwa wanajeshi wa Marekani katika sehemu mbalimbali za Asia Magharibi, Moscow imetoa maonyo makali ya kidiplomasia kwa Washington kuhusu matokeo mabaya ya hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran. Msimamo huu, ambao ulitolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia na Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov, unasisitiza upinzani mkubwa wa Moscow wa kutatua mgogoro wa sasa kati ya Marekani na Iran kwa njia ya mabavu na ya kijeshi na unaweza kutathminiwa ndani ya mfumo wa maslahi ya kimkakati ya Russia yenye pande nyingi. Sababu kuu za msimamo wa Russia zinaweza kuchunguzwa katika maeneo kadhaa muhimu.

Rais Donald Trump wa Marekani

Sababu ya Kwanza, ni kudumisha mshirika muhimu wa kimkakati katika Asia Magharibi. Iran, kama mshirika wa kisiasa, kijeshi, na kiuchumi, ina jukumu muhimu katika milingano ya kikanda, na inahesabiwa kuwa mshirika wa kikmkakati wa Russia katika kukabiliana na ushawishi wa Magharibi. Ukosefu wowote wa utulivu nchini Iran utadhoofisha mhimili wa muqawama dhidi ya Magharibi unaoungwa mkono na Russia na kubadilisha usawa wa nguvu kwa hasara ya Moscow. Ushirikiano wa pande mbili, ikiwa ni pamoja na uungaji mkono wa kidiplomasia wa Russia kwa Iran katika majukwaa ya kimataifa na ushirikiano wa kiulinzi na Iran, unaweza kutathminiwa kutoka pembe hii.

Sababu ya Pili, kuepuka migogoro mipya ya usalama katika eneo la Asia Magharibi na hata kimataifa. Maafisa wa Russia wameweka wazi kwamba, chaguo la kijeshi si tu halitatatua matatizo yaliyopo, bali litazidisha na kuharibu utulivu wa kudumu. Kwa kuwa Russia imo katika mgogoro wa Ukraine, kuenea mgogoro mpya na mkubwa katika Asia Magharibi utakuwa mzigo mzito wa usalama na kijeshi kwa Moscow.

Zaidi ya hayo, Russia ina wasiwasi kuhusu matokeo ya kutokuwa na utulivu unaosababishwa na vita. Mgogoro wa kijeshi unaweza kuathiri ukanda mzima wa Asia Magharibi na kuhatarisha usalama wa nishati na njia za biashara. Kwa hivyo, Russia inasisitiza diplomasia na upatanishi, ikiwa ni pamoja na jukumu la Oman, ili kuzuia hali hiyo isiharibike. Katika suala hili, Lavrov amesisitiza hitajio la kuendelea mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Iran na Marekani ili kufikia makubaliano yanayokubalika kwa pande zote.

Wawakilishi wa Iran na Marekani katika mazungumzo ya nyuklia

Sababu ya Tatu, ni kupinga ushawishi wa Marekani na hatua za upande mmoja za Washington, ambazo zimedhihiri zaidi katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump. Hapo awali Russia ililaani vikali uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Iran na imesema tishio lolote la kijeshi la Marekani kwa kisingizio cha suala la nyuklia la Iran katu halikubaliki. Maonyo haya ni sehemu ya mbinu jumla ya Moscow ya kupinga sera za kibabe za utawala wa Washington na kujaribu kuunda utaratibu wa kimataifa wenye pande nyingi ambapo Umoja wa Mataifa una uzito zaidi pamoja na mataifa kama Russia na China.

Na hatimaye, kudumisha utulivu katika mipaka ya kusini mwa Russia pia ni sababu muhimu ya msimamo huu. Ukosefu wowote wa utulivu nchini Iran unaweza kuwa na athari mbaya kwa hali ya usalama, kijamii, na kiuchumi katika Caucasus na Asia ya Kati, ambayo yanachukuliwa kuwa maeneo ya nje yaliyo karibu na Russia. Kwa hivyo, kudumisha utulivu na amani katika maeneo ya jirani ya Russia kunaendana na maslahi makuu ya usalama ya Moscow.

Kwa ujumla, maonyo ya hivi karibuni ya Russia kuhusu uwezekano wowote wa uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran yanapaswa kuchambuliwa katika muktadha wa mkakati wake mkuu wa kudumisha mshirika muhimu yaani Iran, kupata faida za kijiografia, kuzuia kuibuka migogoro sambamba, na kudhoofisha ushawishi wa Marekani. Msimamo wa Russia unaonyesha kwamba, kwa mtazamo wa Moscow, usalama na utulivu wa Iran una mafungamano yasiyotenganishika na maslahi na usalama wa kitaifa wa Russia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *