Mkutano ujao wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika utaanza Jumamosi, Februari 14, 2026, huko Addis Ababa. Mkutano huu uliandaliwa mapema na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama, ambao walikutana siku ya Jumatano na Alhamisi. 

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu maalum huko Addis Ababa,

Ndani ya mfumo huu, wanachama wa Baraza la Amani na Usalama la AU walifanya mkutano mahususi siku ya Alhamisi kuhusu Somalia na Sudan: wakati vita vikiendelea kupamba moto na maelfu ya raia wameuawa na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Jenerali Hemedti huko El Fasher , baadhi ya nchi zinatetea kuunganishwa rasmi kwa Sudan katika Umoja wa Afrika. Msimamo unaungwa mkoo na baadhi na kupingwa na wengine.

Misri kwa sasa inashikilia urais wa zamu wa Baraza la Amani na Usalama la AU (PSC). Waziri wake wa mambo ya nje, Badr Abdelatty, anafanya kampeni ya kuiunga mkono Sudan kujiunga tena na Umoja wa Afrika. Sudan ilisimamishwa katika Umoja wa Afrika tangu mapinduzi ya Jenerali Al-Burhan mwaka wa 2021. “Lazima tuisikilize Sudan, tuwasikilize wawakilishi wa serikali halali ya Sudan. Kuwaacha au kuwapuuza hakutatui tatizo. Lazima tushirikiane na tuchukuwe maamuzi.”

Waziri wa mambo ya nje wa Misri alimwalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Mohieddine Salem kwenda Addis Ababa, ambapo aliweza kutetea kesi yake na ile ya serikali yake.

Chaguzi na utaratibu wa kikatiba

Lakini nchi nyingi zinapinga kurejeshwa kwa Sudan katika Umoja wa Afrika. “Kuandaa uchaguzi na kurudi kwa utaratibu wa kikatiba ni sharti,” kilieleza chanzo cha kidiplomasia kilichoshiriki katika mkutano huo. Mchunguzi mmoja mwenye uzoefu amebainisha kuwa, katika muktadha wa sasa, kufanyika kwa uchaguzi ni hatua ambayo haitaonesha picha nzuri kwa Sudan, kwaniJenerali Al-Burhan hachukuliwi kuwa halali na nchi zote wanachama.

Katika taarifa yake ya mwisho, Baraza la Amani na Usalama (PSC) lililaani vurugu dhidi ya raia zilizofanywa na wanamgambo wa Vikosi vya Msaad wa Haraka (RSF), lilitoa wito wa kutotambuliwa kwa “serikali yao sambamba,” na, kinyume chake, lilikaribisha mipango ya amani ya serikali ya mpito na kurudi kwake Khartoum. Hata hivyo, halikutaja suala la kurejeshwa tena kwa Sudan katika Umoja wa Afrika.

Mnamo Februari 9, 2026, Sudan ilirejeshwa katika jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), ambapo ilijiondoa yenyewe mwaka wa 2024. Wakati huo, serikali iliona jaribio la upatanishi lililoanzishwa na IGAD kati ya serikali na RSF kuwa ukiukaji wa uhuru wake.

Somaliland

Katika mkutano huu, ambao pia uliijadili Somalia, Baraza la Amani na Usalama lilirudia “kulaani na kukataa kwake bila shaka, kwa maneno makali, kwa utambuzi wa upande mmoja wa Israel wa kile kinachoitwa Jamhuri ya Somaliland.” Utambuzi huu unachukuliwa kama shambulio dhidi ya uadilifu wa eneo la Somalia na tishio kwa amani barani Afrika.

PSC pia “inakaribisha mafanikio ya hivi karibuni yaliyopatikana dhidi ya Al Shabab” na Vikosi vya Usalama vya Somalia, kwa usaidizi wa AUSOM (Kikosi cha Usaidizi na Utulivu ya Umoja wa Afrika nchini Somalia), na inahimiza “mchakato wa ujenzi wa serikali,” ikibainisha haswa “hatua ya kihistoria inayowakilishwa na kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa kitaifa wa manispaa nchini Somalia mnamo mwezi Desemba 2025.”

Wajumbe wapya wa Baraza la Amani na Usalama (PSC)

PSC pia ilichagua wanachama wake kwa muhula wa 2026-2028: Benin, Gabon, Lesotho, Morocco, Somalia, na Afrika Kusini walichaguliwa kama wanachama wapya. Muhula wa Côte d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sierra Leone, na Uganda uliongezwa. Mazungumzo yalikuwa “magumu,” kulingana na washiriki kadhaa. Wakuu wa nchi na serikali wa AU wataidhinisha rasmi muundo huu mpya katika mkutano wao wa kilele siku ya Jumamosi, Februari 14, na Jumapili, Februari 15, katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *