Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ameiomba serikali ya Marekani iishinikize Misri ipunguze hatua za kujizatiti kijeshi katika eneo la Peninsula ya Sinai. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Jumamosi na tovuti ya habari ya nchini Marekani ya Axios.

Axios imeandika: “maafisa wa Israel wanasema kujizatiti kijeshi Misri huko Sinai kumekuwa hatua nyingine muhimu ya mvutano kati ya nchi hizo wakati vita vya Ghaza vikiwa vinaendelea”.

Tovuti hiyo ya habari imemnukuu afisa mmoja wa Marekani na maafisa wawili wa utawala wa kizayuni wa Israel, na kuripotiwa kuwa Netanyahu alimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, -wakati walipokutana siku ya Jumatatu mjini Baitul Muqaddas (Jerusalem)-, orodha ya harakati zinazofanywa na Misri huko Sinai ambazo alidai, zinakiuka kwa kiasi kikubwa makubaliano ya ‘amani’ ya 1979 iliyofikia na Israel, ambayo Marekani ndiye inayoyadhamini.

Makubaliano hayo ya Camp David yaliyofikiwa kati ya Misri na Israel yalitiwa saini mjini Washington mwaka 1979 na Rais wa Misri wa wakati huo Anwar Sadat na waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wakati huo Menachem Begin.

Chini ya mkataba huo, Peninsula ya Sinai iligawanywa katika maeneo maalumu ya kijeshi yenye mipaka tofauti kwa askari na silaha wa Misri na Israel.

Kwa mujibu wa Axios, maafisa wawili wa utawala wa kizayuni wamesema Misri imekuwa ikipanua miundombinu ya kijeshi, “ambayo baadhi yake inaweza kutumika kwa ajili ya kufanyia mashambulio” katika maeneo ambayo silaha nyepesi pekee ndizo zinazoruhusiwa chini ya mkataba huo.

Hata hivyo, afisa mmoja wa Misri, kama alivyonukuliwa na tovuti hiyo ya habari amekanusha madai hayo ya utawala haramu wa Israel na kueleza kwamba, serikali ya Trump “haijazungumzia hivi karibuni suala hilo na Misri”, kama inavyodai Tel Aviv…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *