Qatar imesema kuwa Israel inapasa kuomba radhi kutokana na mashambulizi iliyotekeleza dhidi ya Doha. Imesema Israel inapasa kuomba radhi kama sharti ili kuweza kuanza tena mazungumzo ya amani ya kuhitimisha vita na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo katika Ukanda wa Gaza.

Israel tarehe 9 mwezi huu ilitekeleza mashambulizi huko Doha, mji mkuu wa Qatar na kuuwa wanachama watano wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), lakini viongozi muhimu wa Hamas walinusurika na hujuma hiyo ya Israel. 

Doha inasisitiza kuwa Israel ilitekeleza mashambulizi hayo wakati Qatar ikiwa mwenyeji wa mazungumzo rasmi yenye lengo la kuhitimisha vita vya Gaza. 

Duru mbili za habari ambazo hazikutajwa majina zimeiambia tovuti ya habari ya Marekani ya Axios kwamba Qatar imetaka Israel iombe radhi kwa mashambulizi iliyofanya dhidi ya Doha na irejee kwenye meza ya mazungumzo kujadili makubaliano ya amani na Hamas. 

Doha ambayo ni muitifaki wa Hamas na Marekani pia imekuwa ikizisuluhisha harakati ya Hamas yenye makao yake huko Gaza na utawala wa Tel Aviv. 

Kabla ya kushambuliwa Doha, Mjumbe Maalum wa Rais Donald Trump wa Marekani  Steve Witkoff alitangaza kuwa nchi hiyo inakatisha mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza na kuirudisha nchini timu yake ya mazungumzo kutoka Qatar.

Naye mwakilishi muhimu katika timu ya mazungumzo ya serikali ya Trump kwa jaili ya amani ya Gaza ameulaumu upande wa Marekani na Israel kwa kufeli mazungumzo hayo na Hamas. 

Wakati huo huo Doha inapanga kuchukua hatua za kisheria katika mahakama za kimataifa kulalamikia mashambulizi ya Israel dhidi yake. Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani alisisitiza mapema mwezi huu kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti katika kufuatilia kisheria mashambulizi Israel. ameitaja hatua ya Israel ya kuishambulia Doha kuwa ni “ugaidi wa kiserikali.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *