Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akijibu mshangao wa Rais wa Marekani kuhusu sababu za Iran kutokubali kusalimu amri, aliandika kwa uwazi: “Hatusalimu amri kwa sababu sisi ni Wairani.”

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ameandika katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X akijibu kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump aliyeshangazwa na msimamo kutosalimu amri Iran: “Unataka kujua kwa nini hatusalimu amri? Kwa sababu sisi ni Wairani.”

Kauli hiyo imekuja baada ya mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, Steve Witkoff, kusema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameonyesha mshangao mkubwa kuhusu sababu zinazofanya Iran isikubali masharti ya Washington katika mazungumzo yanayohusu mpango wake wa nyuklia.

Akizungumza katika mahojiano na Lara Trump kwenye kituo cha Fox News, Witkoff amesema kuwa Trump alionekana kukerwa na msimamo imara wa Iran wa kutosalimu amri. Witkoff alidokeza wazi kuwa Trump alidhani Iran inapaswa kulegeza msimamo wake kutokana na shinikizo kubwa linaloikabili.

Kutokubali kwa Iran kusalimu amri mbele ya Marekani kunaweza kuelezewa kwa kuzingatia ngazi tatu za kidhana: ngazi ya kitaifa, kikanda, na kimataifa. Katika muktadha huu, msimamo wa Iran haupaswi kuonekana kama mwitikio wa muda mfupi dhidi ya shinikizo au vitisho, bali kama matokeo ya mantiki iliyojiimarisha kihistoria, kitamaduni, kijiografia‑kisiasa (jiopolitiki), na kimaadili.

Iran ni taifa ambalo katika historia yake ndefu limekabiliwa mara nyingi na uvamizi na uingiliaji wa nguvu za kigeni, lakini halijawahi kuporomoka au kupoteza utambulisho wake wa msingi. Kuanzia mapambano dhidi ya falme na himaya za kale, hadi enzi ya ukoloni mamboleo na kipindi cha kisasa, fahamu ya kitaifa ya Wairani imejengwa juu ya dhana ya kusimama imara dhidi ya ubeberu na satwa ya ajinabi..

Historia hii imefanya fikra ya Muqawama au mapambano  kuwa sehemu ya msingi ya utamaduni wa kisiasa na kijamii wa Iran. Kwa wananchi wa Iran, Muqawama si kauli ya muda au mbinu ya kisiasa, bali ni alama ya heshima (izzah), utu, na sharaf ya taifa.

Ndani ya mfumo huu wa utamaduni wa kitaifa na mshikamano wa ndani, aina yoyote ya kusalimu amri mbele ya shinikizo la nje, hasa kutoka kwa dola ambalo katika kumbukumbu ya pamoja ya taifa la Iran inahusishwa na sera za kupindia serikali, vikwazo vya kiuchumi, na vitisho vya moja kwa moja, hutazamwa kama ukiukaji wa utambulisho wa kihistoria wa Iran.

Steve Witkoff

Ni muhimu pia kuashiria ukweli kwamba katika eneo la Magharibi mwa Asia, ambapo mahusiano kati ya nchi mara nyingi si imara na hutegemea mashindano ya kikabila, kidini, na kijiopolitiki, Iran imeendelea kuwa mhusika wa msingi na muhimu wa siasa za eneo. Tofauti na baadhi ya mataifa, Iran haijawahi kuhitaji kutii au kujifungamanisha kikamilifu na madola makubwa ili kulinda maslahi yake ya kitaifa.

Aidha, jiografia ya kisiasa ya Iran, kuanzia ushawishi wake katika Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz, hadi ukaribu wake na Asia ya Kati na eneo la Caucasus, imeifanya nchi hii kuwa katika kiini cha njia za nishati, biashara, na migogoro ya kiusalama ya kikanda na kimataifa.

Mielekeo ya Iran ya kuimarisha umoja katika sera ya nje, pamoja na msisitizo juu ya uhuru wa ndani na upinzani dhidi ya uwepo wa ajinabi, inatambulika kama vipengele vyenye ushawishi mkubwa katika mahusiano ya kikanda ya Tehran na mataifa mengine. Mwelekeo huu, kwa nchi nyingi za eneo hilo, umejitokeza kama mfano wa harakati za kujitegemea, unaosisitiza uhuru wa maamuzi ya kitaifa na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa misingi ya maslahi ya pamoja badala ya utegemezi kwa madola ya nje.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vilevile, imekuwa mstari wa mbele katika kutetea mataifa yaliyoonewa na kudhulumiwa katika eneo, yakiwemo Palestina, Yemen na Lebanon, na imecheza jukumu muhimu na lenye athari katika kukabiliana na tamaa na upanuzi wa ushawishi wa mhimili wa Marekani–Kizayuni katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Katika ngazi ya kimataifa, Iran inajitazama kama taifa linalosimama dhidi ya mfumo wa kimataifa kibeberu na usio wa haki. Tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, Tehran imejenga sera yake ya nje juu ya kanuni ya “Si Mashariki, si Magharibi” (La Sharqiyya wa La Gharbiyya), ikimaanisha kwamba hakuna dola au nguvu yoyote iliyo na haki ya kulazimisha matakwa yake juu ya taifa la Iran.

Katika miongo ya hivi karibuni, Iran kupitia uwekezaji mkubwa na wa kimkakati katika uwezo wake wa ulinzi, kisayansi na kiteknolojia, imefanikiwa kujenga aina ya nguvu madhubuti ya kuzuia. Maendeleo katika makombora yaliyoundwa ndani ya nchi, ndege zisizo na rubani za kivita, teknolojia ya nyuklia, pamoja na uwezo wa kimtandao ni miongoni mwa viashiria muhimu vya uwezo huu wa kimkakati. Kwa mtazamo wa Iran, uwezo huu hauna lengo la uchokozi, bali kwa ajili ya kulinda mamlaka ya kitaifa, kuhifadhi usalama wa ndani, na kuzuia uingiliaji au mashinikizo ya nje.

Kutokubali kwa Iran kujisalimisha ni zao la busara,  imani na utamaduni wa jamii, nafasi yake mahsusi ya jiopolitiki, uwezo wake wa kujilinda, pamoja na doktrini ya kisiasa ya kutetea uhuru na kujitegemea.

Kwa mtazamo wa Iran, mashinikizo za nje, hasa yale yanayotoka Marekani, si tu kwamba hayajadhoofisha azma ya taifa, bali katika hali nyingi zimeiiimarisha zaidi.

Kwa mtazamo wa Iran, kukubali madai ya kulazimishwa na Marekani kunamaanisha kupoteza uhuru wa kitaifa, heshima na hadhi ya taifa (izzah), pamoja na mizani ya kimkakati katika mazingira ya kikanda na kimataifa. Kwa msingi huo, hakuna serikali yoyote ya Iran, itakayokuwa tayari kukubali hali kama hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *