
Maandamano yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen-Z ya kushinikiza kuboreshwa huduma hospitalini na shuleni yameenea katika miji mbali mbali ya Morocco.
Kwa mujibu wa mashahidi na vikundi vya kutetea haki za binadamu, makumi ya waandamanaji wamekamatwa na kuzuiliwa na maafisa usalama katika miji ya Rabat, Casablanca, Agadir, Tangier, na Oujda.
Maandamano hayo yameripotiwa kuratibiwa mtandaoni na vuguvugu la “GenZ 212,” kundi la vijana ambalo linatumia mitandao ya TikTok, Instagram, na Discord kuhamasisha wafuasi.
Mtandao mwingine, Morocco Youth Voices, pia umewataka washiriki waendelee kujitokeza barabarani, kushiriki maandamano na mikusanyiko ya amani kwa lengo la kuibua mjadala kuhusu sera za kijamii.
Maandamano hayo yalianzia huko Agadir kutokana na hali mbaya na huduma mbovu katika hospitali za umma, na kuenea haraka kupitia mitandao ya kijamii hadi miji mingine ya nchi.
Kwa mujiibu wa Chama cha Haki za Kibinadamu cha Morocco, kama ilivyotajwa na shirika la habari la Associated Press, zaidi ya watu 120 wamezuiliwa tangu maandamano hayo yaanze.
Waziri Mkuu wa Morocco, Aziz Akhannouch, ambaye pia anahudumu kama Meya wa Agadir, ametetea rekodi ya serikali yake, akisema maandamano hayo yamechochewa kisiasa.
Maandamano kama hayo yanayoongozwa na vijana yametikisa nchi nyingine duniani katika miaka na miezi ya hivi karibuni. Nchini Madagascar, maandamano kuhusu uhaba wa umeme na maji yalisababisha kuvunjwa kwa serikali siku ya Jumatatu.