
Rais wa Niger, Abdourahamane Tchiani amesema ulinzi na usalama ni nguzo kuu ya Shirikisho la Muungano wa Nchi za Sahel (AES), huku jumuiya hiyo ikijiandaa kuunda kikosi cha pamoja cha majeshi ya nchi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Koulouba mjini Bamako mwishoni mwa ziara yake ya saa 24 katika mji mkuu huo wa Mali jana Jumanne, Jenerali Tchiani amesema viongozi wa AES wamedhamiria “kuunda na kuimarisha kikosi kilichounganishwa ambacho wakuu wake watafanya kazi kwa pamoja.”
Amesisitiza kwamba, “maswala yote ya ulinzi na usalama yatashughulikiwa na wafanyakazi wa kikosi hiki cha pamoja,” ambacho makao yake kipo Niamey, mji mkuu wa Niger.
Diplomasia na maendeleo ni mihimili mingine miwili ya shirikisho hilo, ameongeza Tchiani akisisitiza kuwa, “ili kuunganisha mihimili hii mitatu, tunakutana kupitia miundo iliyopo ili kutathmini maendeleo yaliyopatikana na malengo yaliyofikiwa.”
Kuhusu diplomasia, AES inasalia “katika msimamo mmoja na inazungumza kwa sauti moja” katika Umoja wa Mataifa na katika majukwaa yote, amebainisha Rais wa Niger, Abdourahamane Tchiani.
Ikumbukwe kuwa, Julai mwaka huu, Muungano wa Mataifa ya Sahel, AES, ulitangaza uzinduzi wa kadi ya utambulisho (kitambulisho) ya pamoja inayotumia teknolojia ya kibiometri.
Muungano huo ulianzishwa rasmi Septemba 2023 na Burkina Faso, Mali, na Niger kama mkataba wa pamoja wa ulinzi na ushirikiano baada ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa katika mataifa hayo. Tangu wakati huo, nchi hizo zinazoongozwa na serikali za mpito za kijeshi zimejiondoa kutoka jumuiya ya ECOWAS, zikiitaja kuwa chombo cha ushawishi wa mkoloni wa zamani, Ufaransa, na tishio kwa uhuru wao; na pia katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kusema mahakama hiyo ni chombo cha ubeberu cha “Ukoloni Mamboleo”.