Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Mariam mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
Kusini mwa Jangwa la Sahara imeshuhudia kushuka kwa viwango vya amani katika mwaka uliopita, ambapo wastani wa hali ya amani katika eneo hili ulipungua kwa asilimia 0.17.
Ingawa baadhi ya mataifa yamepiga hatua kuelekea amani, nusu nyingine ya nchi za eneo hili zimeendelea kudidimia.
Kwa sasa, nchi tatu kati ya kumi zenye migogoro mikubwa zaidi duniani zinapatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kulingana na Ripoti ya Amani ya Dunia ya 2025 (GPI), idadi ya migogoro ya kanda imefikia kiwango chake cha juu zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia, na migogoro mingine mitatu iliibuka mwaka huu pekee.
Nchi nyingi zinajibu kwa kuimarisha majeshi yake.
1. DR Congo
Chanzo cha picha, Getty Images
Eneo hili linakumbwa na changamoto kubwa za kiusalama, hasa kuongezeka kwa machafuko ya kisiasa na ugaidi, hasa katika eneo la Saheli ya Kati.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndiyo nchi inayoongoza kwa ukosefu wa amani katika ukanda huu, na pia imeonesha hali mbaya zaidi kwa mwaka huu.
Kulingana na ripoti ya GPI ya 2025, DRC ni miongoni mwa nchi tano zenye hali mbaya kabisa ya amani duniani.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, DRC imeshuhudia kuporomoka kwa viwango vya amani katika nyanja zote kuu za tathmini, na jumla ya upungufu wa asilimia 4.5.
Nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na vita dhidi ya waasi wa M23, kundi ambalo linadaiwa kuungwa mkono na baadhi ya vikosi kutoka Rwanda.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kuna kati ya wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanaoshiriki katika mapigano ndani ya DRC, wakishirikiana na waasi dhidi ya majeshi ya serikali ya Congo.
2. Sudan Kusini
Kwa upande mwingine, Sudan kusini imeorodheshwa kama nchi isiyo na amani kabisa katika ukanda huu, na pia ni ya tatu miongoni mwa mataifa yasiyo na amani zaidi duniani.
Katika mwaka mmoja uliopita, hali ya amani Sudan kusini ilishuka kwa asilimia 0.54, hasa kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya silaha nzito na za nyuklia.
Lakini furaha ya kupata uhuru ilitoweka mara baada ya mzozo wa kuwania madaraka kati ya Rais Salva Kiir na naibu wake Riek Machar kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyogharimu maisha ya takriban watu 400,000 na kuwalazimu watu milioi 2.5 kukimbia makazi yao.
Hata hivyo, mzozo sasa umeanza tena huko pia, huku Umoja wa Mataifa (UN) ukionya kwamba mkataba wa amani wa 2018 kati ya Kiir na Machar unakabiliwa na tishio la kuvunjika.
Umoja wa Afrika (AU) hadi sasa umeshindwa katika juhudi zake za kurejesha mchakato wa amani, wakati Uganda imetuma wanajeshi wake Sudan Kusini ili kuimarisha nafasi ya Kiir.
Chama cha Machar kinasema hatua hiyo inadhoofisha uhuru wa Sudan Kusini, na makubaliano ya amani ya 2018.
Uganda na serikali ya Kiir inatetea uamuzi huo ikisema inaimarisha makubaliano ya muda mrefu ya usalama kati ya mataifa hayo mawili.
Hata hivyo, wadadisi wanasema hatua hiyo inaonyesha jinsi nguvu ya Kiir mamlakani ilivyo dhaifu, huku hofu ikiongezeka kwamba vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe vinaweza kuanza tena.
Huku hayo yakijiri katika nchi jirani ya Sudan, vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea kupamba moto, huku Jenerali Dagalo akitangaza kuundwa kwa serikali sambamba.
Hatua yake imekuja licha ya kwamba vikosi vyake vimepoteza udhibiti wa Khartoum baada ya mapigano makali. Mji huo sasa umesalia na magofu baada ya majengo yake kulipuliwa kwa mabomu.
3. Mali
Chanzo cha picha, Feras Kilani/BBC
Kwa mujibu wa ripoti ya Amani ya dunia ya mwaka huu 2025, hali ya maisha nchini Mali imeendelea kuwa ngumu sana, hasa mwezi Julai 2025.
Maeneo kama Timbuktu, Gao, Mopti na Menaka yamekumbwa na ukosefu wa usalama wa muda mrefu.
Watu wanaishi kwa hofu, huduma muhimu kama afya na usafiri zimevurugika kabisa.
Mashambulizi ya silaha, vizuizi vya barabarani, na watu kukimbia makazi yao ni mambo ambayo yamekuwa yakitokea kila siku.
Nchi hii ya Magharibi mwa Afrika imekumbwa na janga la usalama lililosababishwa na wanamgambo wa Kiislamu tangu mwaka wa 2012 moja ya sababu zilizotolewa kwa ajili ya kuteka madaraka kijeshi lakini mashambulizi kutoka kwa vikundi vya wanamgambo wa jihadi yanaendelea na hata kuongezeka.
Wiki moja iliyopita kulikuwa na uvumi kuhusu njama ya mapinduzi ya kijeshi.
Hata hivyo, Jenerali Mohammedine alithibitisha kwamba “wanaoshukiwa kupanga njama ya kutetemesha utawala ndani ya vikosi vya usalama vya Mali” wamewekwa kizuizini kwa kujaribu “kuharibu taasisi za jamhuri.”
4. Burkina Faso
Chanzo cha picha, AFP
Tangu mwaka 2015, Burkina Faso imekuwa katika mzozo unaozidi kuwa mbaya unaochochewa na wanamgambo wa Kiislamu, hasa katika maeneo yake ya kaskazini na mashariki yanayopakana na Mali na Niger.
Uasi huu, ambao awali ulikuwa ni matokeo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Mali mwaka 2012, umezidi, huku vikundi kama Jama’at Nusrat al-Islam wal Muslimeen (JNIM), Dola la Kiislamu katika Sahara Kuu (ISGS), na Ansaroul Islam wa Burkina Faso wakitumia malalamiko ya ndani, mvutano wa kikabila, na ukosefu wa utawala mzuri kufanya uhalifu.
Kufikia mwaka 2025, takriban asilimia 60 ya eneo la Burkina Faso inaripotiwa kuwa nje ya udhibiti wa serikali, huku vikundi vya jihadi vikifanya mashambulizi katika vituo vya jeshi, makazi ya watu, na miundombinu muhimu.
Kufikia Agosti, zaidi ya watu milioni 2.3 walikuwa tayari wamekimbia makazi yao wengine wakitafuta hifadhi ndani ya nchi, na wengi wakikimbilia mataifa jirani.
Familia zimetawanyika, watoto wamekatishwa masomo, na wengi wanaishi kwa hofu ya kesho isiyojulikana.
Haya ni kwa mujibu wa tathmini ya usalama Africa ASA.
5. Somalia
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa Somalia, hali ya usalama imeendelea kuwa tete.
Kundi la Al-Shabab limekuwa likitekeleza mashambulizi mabaya kwa kutumia mabomu, mashambulizi ya kujitoa mhanga, na hata kuwalenga watu maalum kwa mauaji.
Mamia ya raia wameuawa, na wengi kujeruhiwa.
Mnamo Agosti 2, kundi hilo lilishambulia mgahawa mmoja wa ufukweni jijini Mogadishu, na kuua watu 37, huku zaidi ya 200 wakijeruhiwa.
Wengi waliokufa walikuwa wakila au kufanya kazi raia ambao walikuwa wakijishughulisha na maisha yao katikati ya machafuko.
Serikali nayo ilijibu kwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Al-Shabab, lakini hata hayo yaliwaumiza raia.
Mnamo Machi 18, mashambulizi ya anga yaliyoungwa mkono na ndege zisizo na rubani kutoka Uturuki yaliwaua raia 23, wakiwemo watoto 14, karibu na kijiji cha Bagdad haya ni kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.
Ni eneo ambalo limekuwa kitovu cha mapigano kwa miezi mingi.
Marekani pia ilikiri kushiriki mashambulizi ya anga kusaidia jeshi la Somalia.
Machafuko mengine yalitokana na migogoro ya kimakabila, hasa katika jimbo la Galmudug, ambako upungufu wa maji, malisho, na ardhi ulichochea mapigano.
Wakati huo huo, Al-Shabab wanaendelea kuua watu wanaodhaniwa kushirikiana na serikali au vikosi vya kigeni.
Ni hali ya hofu isiyoisha, ambapo hakuna anayehisi yuko salama hata wale wasiokuwa na hatia.
6. Jamhuri ya Kati ya Afrika
Hali si tofauti katika Jamhuri ya Kati ya Afrika.
Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) wameendelea kuathirika na mapigano kati ya makundi hasimu tangu Muungano wa Wazalendo wa Mageuzi (CPC) ushirikiano wa kiholela wa makundi yenye silaha ya uporaji ulipoanzisha mashambulizi dhidi ya serikali mwishoni mwa mwaka 2020.
Mashambulizi hayo yalivuruga makubaliano ya amani ya mwaka 2019, ambayo yalikuwa yamehitimisha rasmi zaidi ya miaka mitano ya vita vya silaha.
7.Nigeria
Chanzo cha picha, KADUNA STATE GOVERNMENT
Takwimu zilizomo katika ripoti ya Amani duniani 2025 kuhusu “mtazamo wa uhalifu na uzoefu wa ukosefu wa usalama nchini Nigeria” ni za kutisha.
Utafiti huu uliozinduliwa hivi majuzi unaonyesha kuwa Nigeria imeorodheshwa ya saba kuwa nchi hatari kusihi barani Afrika.
Ripoti hii inajiri kufuatia mwezi Septemba mwaka jana, baada ya wanamgambo wa Boko Haram kushambulia mji wa Mafa huko Yobe, kaskazini mashariki mwa Nigeria, ilirudisha hofu ya enzi ambayo wakazi walidhani imepita.
Uhalifu katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
Katika upande wa jumuiya ya Afrika mashariki Kenya inaongoza katika taifa lisilo na usalama zaidi likiorodheshwa nafasi ya 14 barani Afrika.
Uganda nayo ikitajwa nafasi ya 23 kwa nchi isiyo salama na kuifanya ya pili katika jumuiya ya Afrika mashariki.
Nchi jirani ya Tanzania ikitajwa nchi salama kuishi kwa kuorodheshwa nafasi ya 73 duniani.Kutokana na tathmini hiyo Tanzania ina viwango vichache vya uhalifu katika jumuiya ya Afrika Mashariki.
Takwimu za kushangaza
Amani duniani imeendelea kudorora kila mwaka tangu 2014.
Katika kipindi hicho, nchi 100 zimeshuhudia kushuka kwa viwango vya amani, huku ni nchi 62 pekee zilizoboresha hali zao.
Tofauti kati ya mataifa yenye amani kubwa na yale yenye migogoro imezidi kupanuka, ambapo ukosefu wa usawa katika amani umeongezeka kwa asilimia 11.7 katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.
Nchi 25 zilizo tulivu zaidi zimerekodi kupungua kwa amani kwa wastani wa asilimia 0.5, huku nchi zisizo na utulivu zikiporomoka kwa asilimia 12.2 katika kipindi hicho.
Vifo kutokana na migogoro ya ndani vimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 438 katika miaka 17 iliyopita.
Katika mwaka mmoja uliopita, nchi 75 kati ya zile zilizopimwa na GPI ziliripoti angalau kifo kimoja kutokana na mapigano ya ndani.
Kwa sasa, zaidi ya watu milioni 122 wamelazimika kuhama makazi yao kwa nguvu.
Kuna nchi 17 ambako zaidi ya asilimia tano (5%) ya wakazi wake ni wakimbizi au watu waliotawanywa ndani ya nchi zao.
Idadi ya waliolazimika kuhama kwa nguvu imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 185 tangu kuanzishwa kwa Kiashiria cha Amani Duniani (GPI).