
Arsenal ina mpango wa kufanya maboresho makubwa Uwanja wake wa Emirates uliopo London, England, ambayo yatafanya ihamie kwa muda katika Uwanja wa Wembley ambao nao upo London.
Lengo la maboresho hayo ni kuongeza ukubwa utakaoufanya iingiza mashabiki 70,000 kutoka idadi ya mashabiki 60,704 wanaoingia hivi sasa.
Kukamilika kwa maboresho hayo kutaufanya Uwanja wa Emirates kushika nafasi ya pili nyuma ya Old Trafford kwa kuingiza idadi kubwa ya watu kama ilivyokuwa wakati ulipozinduliwa.
Mwaka 2006, Emirates ulikuwa unashika nafasi ya pili nyuma ya Old Trafford ambao unaingiza mashabiki 75,000 lakini kwa sasa uko nafasi ya nne kwa upande wa viwanja vya timu ukizidiwa pia na Anfield wa Liverpool unaoingiza mashabiki 61,276, wa Tottenham Hotspur ambao unaingiza mashabiki 62,850 huku wa London unaomilikiwa na West Ham United ikiingiza mashabiki 62,500.
Arsenal inataka kuongeza mapato zaidi kutokana na viingilio vya mashabiki hivyo inaamini itavuna kiasi kikubwa cha fedha baada ya Uwanja huo kuanza kuingiza mashabiki 70,000.
Kiasi cha takribani Pauni 500 milioni (Sh 1.7 trilioni) inaripotiwa kimepangwa kutumiwa na Arsenal kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo.
Inaripotiwa kwamba Arsenal imeshawishika na namna Real Madrid inavyoingiza kiasi kikubwa cha fedha hivi sasa baada ya maboresho makubwa iliyowahi kuyafanya katika Uwanja wake wa Santiago Bernabeu.
Real Madrid iliongeza idadi ya siti 4,000 ambazo ziliufanya uwanja huo uwe na uwezo wa kuingiza mashabiki 83,186 hivi sasa.
Na imepelekea mapato ya viingilio kwa Real Madrid kuongezeka mara mbili ambapo kwa sasa Santiago Bernabeu inaipa Real Madrid takrbani Pauni 215 milioni (Sh709 bilioni).