Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, dhana ya mazoezi imekuwa ikihusishwa zaidi na kupunguza uzito au kutengeneza umbo zuri, Lakini kwa wanawake wengi wa kizazi kipya, mazoezi si tena suala la mwonekano pekee  bali ni njia ya kujenga nguvu , kuimarisha afya ya akili .

Katika ulimwengu wa leo uliojaa presha za kazi, familia, mitandao ya kijamii na matarajio ya jamii, mazoezi yamegeuka kuwa silaha ya mwanamke dhidi ya msongo wa mawazo pia chanzo cha kujiamini, uthubutu na utulivu.

URE 01

Kujiamini kwa mwanamke huanza na namna anavyohisi kuhusu mwili wake, Lakini tafiti nyingi zinaonyesha kuwa si lazima uwe na umbo fulani ili ujihisi vizuri.

Kinachojenga kujiamini zaidi ni kujua una nguvu ya kufanya kitu iwe ni kukimbia kilomita tano, kufanya mazoezi, au hata kupiga push-up.

Dk. Angela Mushi, mtaalamu wa saikolojia wa michezo, anasema: “Mwanamke anapojihusisha na mazoezi mara kwa mara, mwili wake huzalisha kemikali zinazoongeza hali ya furaha na kupunguza wasiwasi, anajihisi mwenye uwezo, mwenye udhibiti wa maisha yake na mwenye thamani zaidi.”

Kujiamini hakuzaliwi kwa kujilinganisha na wengine, bali kwa kuona maendeleo yako binafsi, hivyo kila tone la jasho linakuwa hatua moja kuelekea kujipenda zaidi.

Mazoezi kama  dawa

Kila siku wanawake hukabiliana na changamoto nyingi, ikiwemo majukumu ya kifamilia, presha ya kazi, matatizo ya kifedha, na hata changamoto za kihisia, Wataalamu wanasema mazoezi ni mojawapo ya tiba bora zaidi dhidi ya msongo wa mawazo bila dawa.

Mazoezi huchochea uzalishaji wa kemikali asilia mwilini zinazojulikana kama “feel-good hormones”. Hii ndiyo sababu baada ya kukimbia, kucheza, au kufanya yoga, mtu huhisi utulivu na furaha ya ajabu.

Mwanamke mmoja anayefanya mazoezi anasema: “Nilianza mazoezi kwa sababu nilitaka kupunguza uzito, lakini sasa nafanya kwa sababu yananifanya nijisikie hai. Nikiwa na mawazo, nikienda ‘gym’ ninarudi na tabasamu.”

URE 02

Mazoezi na urembo
Urembo wa kweli haupo kwenye mapambo au mavazi pekee, urembo wa mwanamke huanza ndani kwenye afya yake ya akili, mwili wenye nguvu na ngozi yenye mng’ao unaotokana na afya njema.

Mazoezi huimarisha mzunguko wa damu, kusaidia usingizi na kutoa sumu mwilini, hali inayofanya ngozi ionekane safi na yenye afya.

Kwa wanawake wengi, mazoezi ni njia ya kujiweka sawa kimwili na kiakili bila kutumia gharama kubwa za vipodozi, mchakamchaka wa asubuhi, yoga, au kuogelea ni tiba ya asili inayozidisha mvuto wa asili wa mwanamke.

URE 03

Wanawake mashuhuri
Dunia imejaa mifano ya wanawake mashuhuri wanaothibitisha nguvu ya mazoezi.

Serena Williams, nyota wa tenisi, anaamini mazoezi si tu kwa ushindani bali kwa afya ya akili. Anasema; “Mimi hupata amani yangu ndani ya mazoezi, hapo ndipo napata nguvu ya kuwa mama, mwanamke na bingwa.”

Vanessa Mdee, msanii kutoka Tanzania, amewahi kusimulia jinsi mazoezi na yoga vilivyomsaidia kupambana na msongo wa mawazo. Kupitia video zake, amekuwa akihamasisha wanawake kuwekeza katika afya ya akili zaidi ya muonekano.

Hata wanawake wa kawaida kama kina mama wa nyumbani, wafanyakazi wa maofisini na wanafunzi, wamekuwa wakihusisha mazoezi kama sehemu ya maisha mapya ya kujipenda.

URE 04

Uzuri na afya 
Jamii inabadilika, zamani uzuri wa mwanamke ulipimwa kwa umbo au mavazi, leo uzuri unamaanisha afya, nguvu na utulivu wa akili, wanawake wanajifunza kwamba si lazima uwe pisi kali, bali uwe na furaha na afya.

Kampeni nyingi za kimataifa kama ‘Strong Not Skinny’ (mwenye nguvu si mwembamba) zimekuwa zikiwahamasisha wanawake wa aina zote kupenda miili yao na kufanya mazoezi kwa sababu ya afya, si kwa shinikizo la urembo wa mitandao.

URE 05

Wanachosema wataalamu 
Mtaalamu wa lishe, Dk. Rehema Kasele, anasema: “Mazoezi yanaongeza Oksijeni mwilini, yanapunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, kisukari na matatizo ya homoni kwa wanawake, yanaimarisha mzunguko wa damu, hivyo kuongeza hata afya ya ngozi na nywele.”

Kwa upande mwingine, mshauri wa maisha, Flora Ng’eni, anasisitiza umuhimu wa mazoezi katika kujenga nidhamu ya maisha.

“Unapoweza kujilazimisha kufanya mazoezi hata siku ambazo huna hamasa, unajifunza kujidhibiti, huo ndiyo msingi wa mafanikio katika nyanja zote,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *