Kikao cha kamati ya uongozi wa chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania kimemvua uanachama Monalisa Joseph Ndala, kufuatia hatua yake ya kuwasilisha malalamiko kwa msajili wa vyama vya siasa yaliyosababisha Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kumuengua mgombea wa urais wa chama hicho.
Luhaga Mpina aliyeteuliwa na Chama cha ACT – Wazalendo kuwania urais alienguliwa na INEC kufuatia uamuzi wa ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukubaliana na hoja za Monalisa.
Sababu kuu iliyoelezwa na Monalisa ni kwamba Mpina alipata uanachama Agosti 5, 2025, nje ya muda wa kisheria wa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, ambapo ilipaswa kuwa kabla ya Mei 25, 2025.
Taarifa iliyotiwa saini na kutumwa katika vyombo vya habari na katibu wa tawi la Mafifi mkoani Iringa, Neema Ernest Kivamba, imeeleza kuwa mkutano uliofanyika katika tawi hilo vilevile ulibaini kwamba Monalisa ameshindwa kutekeleza matakwa ya katiba ya chama hivyo basi kupoteza sifa ya kuwa mwanachama wa chama cha ACT – Wazalendo.
‘Kwa barua hii tunakujulisha rasmi kuwa kuanzia leo tarehe 28.08.2025 kamati ya uongozi ya tawi la Mafifi imekuondoa katika orodha ya wanachama wake katika rejista ya tawi na kadi namabri 0000245 iliyokuwa imeandikishwa kwa jina lako ipo wazi na tumeitaarifu idara ya oganaizisheni, Uchaguzi na wanachama wa chama taifa ili iweze kutolewa kwa mwanachama mwengine’, ilisema taarifa hiyo.
Mahakama Kuu ya Tanzania hata hivyo tayari imetoa muda wa siku tano kwa Serikali kujibu hoja zilizowasilishwa na ACT Wazalendo na Luhaga Mpina dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
ACT Wazalendo ilikwenda mahakamani kudai kulikuwa na ukiukwaji wa Katiba, sheria na kanuni za uchaguzi wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea urais uliohitimishwa Agosti 27.
Mahakama imeeleza bayana kuwa endapo itabainika kuwa Tume Huru ya Uchaguzi ilikiuka katiba na sheria, haitasita kutoa amri ya kumpa Mpina fursa ya kurejesha fomu na kushiriki katika uchaguzi wa urais.