Nahodha wa Arsenal, Martin Ødegaard, ataendelea kuwa nje ya uwanja hadi mwezi Novemba kutokana na jeraha la goti.
Nahodha huyo wa kikosi cha Mikel Arteta kinachowania taji la Ligi Kuu ya England, anatarajiwa kukosa kipindi kigumu ambacho Arsenal itakutana na mechi dhidi ya Fulham, Crystal Palace, Burnley, na Sunderland, pamoja na michezo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid na Slavia Prague. Pia mechi ya raundi ya 16 ya Carabao Cup dhidi ya Brighton.
Ødegaard alipata jeraha kwenye goti la kushoto wakati wa ushindi wa 2-0 dhidi ya West Ham kabla ya mapumziko ya kimataifa na nafasi yake ilichukuliwa na Martin Zubimendi, na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kubadilishwa katika kipindi cha kwanza kwenye mechi tatu mfululizo alizoanza katika Ligi Kuu ya England.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, alikuwa anahangaika na jeraha la bega alilopata wakati wa ushindi wa 5-0 dhidi ya Leeds, Agosti 23, 2025, jambo lililosababisha asicheze mechi dhidi ya Liverpool iliyomalizika kwa Arsenal kupoteza bao 1-0.
Ødegaard alionekana kurejea katika hali nzuri na alijiunga na kikosi cha taifa cha Norway mwezi uliopita, ambako alicheza mechi mbili kabla ya kuumia tena dakika chache tu (chini ya dakika 20) katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Nottingham Forest.

Hakucheza katika ushindi wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Athletic Club wala sare ya dakika za mwisho dhidi ya Manchester City, lakini alirejea kwa kiwango kizuri dhidi ya Olympiacos. Hata hivyo, baada ya kugongana na Crysencio Summerville dhidi ya West Ham, alilazimika kutolewa nje ya uwanja kutokana na jeraha la goti.
Baada ya mechi hiyo, Ødegaard alipigwa picha akiwa amevaa kifaa cha kuimarisha goti, huku kocha Arteta akisema kuwa hakujisikia vizuri kuhusu jeraha hilo.
Alijiondoa kwenye kikosi cha Norway kutokana na hali hiyo, ingawa alikuwepo kwenye jukwaa la Uwanja wa Ullevaal jijini Oslo siku ya Jumamosi kushuhudia Norway ikiibuka na ushindi wa 5-0 dhidi ya Israel, katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia, ambapo Erling Haaland alifunga hat-trick.
Kikosi cha Ståle Solbakken kitapambana na New Zealand katika mechi ya kirafiki leo Jumanne, Oktoba 14, 2025 kabla ya mechi za kufuzu dhidi ya Estonia na Italia mwezi Novemba. Kwa mujibu wa ripoti ya BBC, Ødegaard hatahusika na mechi hizo na anatarajiwa kurejea baada ya mapumziko ya kimataifa ya mwezi huo.

Wachezaji wengine wa Arsenal ambao kwa sasa ni majeruhi ni Noni Madueke, Kai Havertz na Gabriel Jesus (wote goti), huku kocha Arteta akitarajia kwamba mchezaji mpya Piero Hincapie, atakuwa tayari kucheza baada ya mapumziko ya kimataifa baada ya kupona majeraha ya nyonga alioyapata mazoezini.
Arsenal itarejea uwanjani Jumamosi wiki hii ikitarajiwa kucheza ugenini dhidi ya Fulham kwenye dimba la Craven Cottage, kabla ya kuwakaribisha Atletico Madrid katika Uwanja wa Emirates, kaskazini mwa jijini London.
Mechi ya kwanza ya Arsenal baada ya mapumziko ya mwezi Novemba itakuwa dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Tottenham (North London Dabi), ikifuatiwa na michezo mikubwa dhidi ya Bayern Munich na Chelsea.