London, England. Pesa kubwa inapotumika, matarajio yake ni makubwa pia. Lakini, kwenye Ligi Kuu England mambo yamekuwa tofauti, wachezaji wanaosajiliwa kwa pesa kubwa, mara chache wamekuwa wakionyesha viwango vikubwa uwanjani.
Katika miaka ya karibuni, dili zote za uhamisho wa wachezaji zilizogharimu pesa nyingi mastaa hao wameshindwa kuzisaidia timu kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu England.
Liverpool ilimfanya kiungo Florian Wirtz kuvunja rekodi ya uhamisho Uingereza wakati ilipomsajili kutoka Bayer Leverkusen wakati wa dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu.
Lakini, wiki chache baadaye, Liverpool ilivunja rekodi nyingine ya uhamisho Uingereza wakati ilipomsajili straika Alexander Isak kutoka Newcastle United kwa ada ya Pauni 125 milioni.
Na presha sasa imempanda straika huyo wa Sweden, ambaye anahesabika kama mmoja wa washambuliaji bora kabisa duniani, kuhakikisha Liverpool inakuwa namba moja.
Historia inaonyesha kwamba kwa miaka ya karibuni, mchezaji ghali zaidi ameshindwa kabisa kuipa timu yake ubingwa. Kwenye orodha ya wakali 10 ghali England ni wawili tu ndiyo waliowahi kubahatika kuzipa timu zao ubing wa wa Ligi Kuu England, lakini nao hawakucheza kwa viwango vilivyotarajiwa na wengi.

Wachezaji hao ni Jack Grealish na Darwin Nunez. Grealish, ambaye ni mkali za zamani wa Aston Villa alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu England baada ya kujiunga na Manchester City kwa uhamisho wa Pauni 100 milioni. Nunez ameachana na Liverpool mwaka huu baada ya miaka mitatu kupita tangu aliponaswa kwa Pauni 85 milioni kutokea Benfica, huku maisha yake ya Anfield yalikuwa na msongo mkubwa wa mawazo kuliko mafanikio.
Isak matumaini yake ni kupata mafanikio kuliko mawazo. Amejiunga na timu inayoonekana kuwa vizuri baada ya kunyakua ubingwa wa ligi msimu uliopita, lakini maisha yake yameanza kwa kasi hafifu sana.
Tayari kikosi hicho cha Anfield chini ya kocha Arne Slot kimekuwa na kiwango cha hovyo katika mechi ambazo staa huyo wa Sweden amekuwa uwanjani, ikipoteza mechi tatu mfululizo.
Isak kwa sasa ndiye mchezaji ghali Uingereza. Kabla yake kulikuwa na Wirtz, ambaye alitua kuvunja rekodi ya kiungo wa Chelsea, Enzo Fernandez. Staa huyo wa Kiargentina, Enzo alitua Stamford Bridge akitokea Benfica kwenye dirisha la Januari akitokea kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia huko Qatar, ambako alitajwa kinda bora wa michuano.
Fernandez alijiunga na Chelsea kwenye dirisha la Januari 2023 kwa ada ya Pauni 105 milioni. Alichobeba hadi sasa ni taji la Europa Conference League na Kombe la Dunia la Klabu. Mchezaji mwenzake huko Stamford Bridge, Moises Caicedo, naye alijiunga kwenye timu hiyo miezi michache baadaye kwa ada inayozidi Pauni 100 milioni.
Caicedo alisaini dili ambalo litapanda hadi kufikia Pauni 115 milioni, ambayo ilikuwa rekodi Uingereza. Ametengeneza kombinesheni bora kabisa na Fernandez kwenye eneo la kiungo, lakini wanasoka hao ghali wanashindwa kuifanya Chelsea kuwa timu ya kushindania ubingwa.
Mchezaji ambaye ameonyesha ubora pia kwa kwenye orodha ya wanasoka ghali ni Declan Rice.

Alijiunga na Arsenal akitokea West Ham kwa ada ya Pauni 100 milioni, ambayo itaongezeka na kufikia Pauni 105 milioni. Kiungo huyo wa England sasa anahesabika kama mmoja wa wachezaji bora kweye ligi katika nafasi yake anayocheza.
Amekuwa na kiwango bora kwenye kikosi cha Arsenal, lakini bado ameshindwa kuipa taji hilo ubingwa wa ligi. Katika miaka yake miwili aliyokuwa Arsenal timu hiyo imemaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Mwaka 2021, Chelsea ilipokuwa chini ya Roman Abramovich ilifanya usajili uliovunja rekodi kwa kutumia Pauni 97.5 milioni ilipomnasa Romelu Lukaku kutoka Inter Milan. Staa huyo alionekana kama straika ambaye angeenda kuipa Chelsea ya Thomas Tuchel taji la ligi. Lakini, staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji hakuna alichokifanya na matokeo yake aliishia tu kutolewa kwa mkopo kabla ya kuondoka jumla kutimkia Italia, ambako alikwenda kushinda mataji ya Serie A akiwa na kikosi cha Napoli na Inter Milan.
Paul Pogba kuna wakati alishikilia cheo cha kuwa mwanasoka ghali duniani, wakati aliponaswa na Manchester United iliyochukua chini ya Jose Mourinho mwaka 2016. Lakini, Mfaransa huyo hakuwa ambacho amefanya kwenye timu hiyo na kushidwa kabisa kuipa taji ya Ligi Kuu England, kabla ya miamba hiyo ya Old Trafford kumsajili mchezaji wao ghali mwingine, Antony kutoka Ajax mwaka 2022. Antony naye hakuna ambacho amefanya cha maana huko Man United na kujikuta akitolewa kwa mkopo kabla ya kuondoka jumla kutimkia Real Betis.