Baada ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Zambia kuwania nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ itashuka dimbani leo Jumanne kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki na Iran kwenye Uwanja wa Shabab Al Ahli, Dubai, Falme za Kiarabu.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mataifa hayo kukutana ambapo kwa mujibu wa viwango vya ubora wa soka duniani vinavyotolewa na Fifa Tanzania inashika nafasi ya 107, huku Iran ni 21.

Tofauti hiyo kubwa ya nafasi inaifanya mechi kuwa kipimo kizito kwa vijana wa Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’.

Taifa Stars na Iran  zinakutana zikiwa zinatoka kupoteza mechi mbili za mwisho katika mashindano tofauti. Kwa upande wa Stars, iliangukia mikononi mwa Niger na Zambia ikipoteza kwa bao 1-0 katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia.

STA 01

Kwa upande mwingine, Iran ilipoteza mechi mbili mfululizo ya kwanza dhidi ya Uzbekistan bao 1-0 katika Kombe la Mataifa ya Asia ya Kati (CAFA Nations Cup) na baadaye kufungwa 2-1 na Russia katika mechi ya kirafiki huko Volgograd.

Akiwazungumzia Wairani mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, ambaye anacheza soka la kulipwa Iraq katika klabu ya Al-Talaba, licha ya kutokuwa sehemu ya kikosi cha Stars, amesema anatambua ubora wa wapinzani lakini anaamini Stars inaweza kuonyesha kiwango bora.

“Mpira unaochezwa kwa mataifa haya ni nguvu na akili, hivyo sioni kama wachezaji wa Taifa Stars watakuwa na wakati mgumu. Naamini tunaweza kufanya vizuri, hii itakuwa mechi nzuri kwetu,” amesema Msuva.

Msuva aliongeza kuwa, mechi hiyo ni fursa kubwa ya kuongeza nafasi ya Tanzania kupanda katika viwango vya FIFA, hasa ikizingatiwa Iran ipo kwenye nafasi za juu na ushindi unaweza kuonyesha kuwa sisi sio wanyonge.

STA 02

Morocco amesema maandalizi yamekamilika na wachezaji wote wapo katika hali nzuri kimwili na kiakili.

“Wachezaji wapo kwenye afya njema, kila mmoja anaonekana yupo tayari kwa mechi hii. Tulicheza dhidi ya Zambia na kupoteza, lakini mechi hii ni tofauti. Ni mechi nyingine yenye changamoto zake na naamini itakuwa mechi nzuri kwa sababu na sisi tumekua,” amesema kocha huyo.

Morocco alifafanua kuwa mechi hiyo ni sehemu ya mchakato wa kujenga timu imara kuelekea mashindano yajayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *