Dar es Salaam. Meneja wa Diamond Platnumz, Mkubwa Fella, amewataka mashabiki kuacha kama yalivyo masuala ya bifu za wasanii kwani hakuna anayejua mwanzo wa kazi zao wala chimbuko la bifu hizo.
Fella ambaye kwa sasa hali yake kiafya inaendelea vizuri huku akizidi kufanya mazoezi ya hapa na pale, ameliambia Mwananchi mashabiki wanapenda kuingilia kati vitu wasivyovijua kiundani, jambo ambalo sio zuri na linaivuruga sanaa.

“Ukweli ni kwamba hawapaswi kungumzia bifu za wasanii, hii inakuwa kama wanachochea wasanii kuwa na bifu milele au kushindwa kufanya kazi zao kwa ufasaha.
“Kwa hiyo hupaswi wewe kama shabiki kuingilia vitu ambavyo huvijui, na niwaambie tu wakati mwingine hawa wasanii huwa wenyewe wanafahamiana vizuri pindi wanapokuwa na mgongano ama huwa wanajua nini wanataka kukifanya kwa wakati huo, kwa hiyo wewe shabiki unaingia kati unaanza kumtetea msanii huyu na kumtukana yule wakati hamfahamu chanzo.”

Mkubwa Fella, amezungumza haya baada ya Mwananchi kumuuliza anachofahamu kuhusu mvutano uliotokea katika mitandao ya kijamii kati ya wasanii Diamond Platnumz na Mbosso hadi kurushiana maneno kwenye mitandao ya kijamii zaidi ya mwezi mmoja uliopita. Wimbo unaotamba ‘Pawa’ wa Mbosso, ulionekana kuwa kitovu cha malumbano yaliyohusisha mashabiki wa pande zote mbili.