
Waziri wa fedha wa utawala wa kizayuni wa Israel katika taarifa yake ya dharau kuhusu Saudi Arabia, amesema kwamba hatakubali makubaliano ya kuuanzisha uhusiano wa kawaida na Riyadh ikiwa kutakuwa na sharti la kuundwa dola huru la Palestina.
Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich alisema jana kwamba ikiwa Saudi Arabia itasema inataka kuanzishwa kwa dola la Palestina mkabala wa makubaliano ya kuanzisha uhusiano na Israel, “tutawaambia: Hapana asanteni, marafiki. Endeleeni kupanda ngamia katika jangwa la Saudia.”
Matamshi ya Waziri huyo wa Kizayuni ambayo yamekabiliwa na ukosoaji mkubwa, yametolewa katika wakati ambapo Rais Donald Trump wa Marekani atarajiwa kuwa mwenyeji wa Mwana Mfalme wa Saudia Mohammed bin Salman katika Ikulu ya White House mwezi ujao.
Kwa mujibu wa gazeti la Times of Israel, katika safari hiyo, Trump anapanga kujadiliana na bin Salman kuhusu uendelezaji wa makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, unaojulikana kama Makubaliano ya Abraham, ambayo UAE na Bahrain zimejiunga nayo hapo awali.
Aidha kwa mujibu wa ripoti hiyo, Riyadh kwa muda mrefu imekuwa ikisema kuwa iko tayari kuufanya uhusiano wake na Israel kuwa wa kawaida tu iwapo Tel Aviv itakubali njia mahususi na ya muda ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina. Hili ni suala ambalo licha ya uungwaji mkono mkubwa duniani na hata kutoka kwa baadhi ya washirika wa Marekani, lakini Israel na mshirika wake mkuu, Marekani, wanalipinga vikali.