
Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamepelekwa nchini Tanzania kwa ajili ya kusimamia zoezi la uchaguzi mkuu wan chi hiyo ulioapnagwa kufanyika Jumatano ijayo Oktoba 29.
Hatua hiyo inafuatia mwaliko wa Serikali ya Tanzania ambao ni sambamba na maagizo ya Baraza la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) linalohitaji Jumuiya hiyo kufuatilia uchaguzi wa nchi zote wanachama.
Kiongozi wa ujumbe huo ambaye pia ni makamu wa rais wa zamani wa Uganda Dkt Speciosa Wandira Kazibwe alizungumza wakati wa uzinduzi wa wa misheni hiyo.
“Kama jumuiya iliyoanzishwa juu ya kanuni za utawala bora, sheria, na heshima kwa haki za binadamu, EAC inazingatia uchaguzi wa kuaminika kama msingi wa demokrasia na ujumuishaji wa kikanda,” alisema Dkt Speciosa Wandira Kazibwe.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa EAC, Mhe. Veronica Nduva, amesema kuwa misheni hiyo itatoa taarifa ya awali muda mfupi baada ya uchaguzi, ikifuatiwa na ripoti kamili ya mwisho. “Ripoti hizi zitawasilisha tuliyobaini na kutoa mapendekezo yenye lengo la kuimarisha michakato ya uchaguzi ya baadaye katika eneo hilo.”
Waangalizi pia watakuwa na fursa ya kutangamana na washikawadau wa uchaguzi, kufuatilia shughuli za kampeni za mwisho, na kufuatilia shughuli hiyo inavyoendelea katika vituo vya kupigia kura, upigaji kura, zoezi la kuhesabu kura, na shughuli ya utangazaji wa matokeo ya uchaguzi huo.
Uchaguzi mkuu wa Tanzania utafanyika siku ya Jumatano, tarehe 29 Oktoba 2025, watu waliotimiza masharti ya kupiga kura watakuwa na fursa ya kumchagua Rais, wabunge na madiwani.
Wapinzani nchini Tanzania wamekuwa wakidai kukandamizwa huku baadhi ya wagombea wao wakizuiwa kugombea nafasi mbalimbali.