Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: Hati ya Umoja wa Mataifa imekumbana na mitihani mingi mizito kutokana na vitendo vya ukatili na kutumiwa vibaya kisiasa ya taasisi zake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Amir Saeed Iravani,  amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumamosi na kusisitiza kwa kusema: “Leo hii, Hati ya Umoja wa Mataifa ambayo ndio msingi wa sheria za kimataifa na ushirikiano wa pande nyingi, imekumbwa na mitihani mingi kutokana na vitendo vya uchokozi vinavyoendelea katika kona mbalimbali duniani na kutokana na kutokujali na kutumiwa vibaya kisiasa mifumo yake. Kuna mifano miwili mibaya ambayo inahitaji umakini maalumu wa Baraza la Usalama. Kwanza, vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na nchi yangu Iran.”

Ameendelea kufafanua mfano huo wa kwanza kwa kusema: “Tarehe 13 Juni, 2025, utawala wa Kizayuni, kwa kusaidiwa moja kwa moja na kwa kushirikiana na Marekani, ulianzisha vita vikubwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya sababu wala kuchokozwa. Sasa kuendelea kukaa kimya Baraza la Usalama na kushindwa kuchukua hatua za kukabiliana na ukiukaji huo mbaya wa hati ya Umoja wa Mataifa si tu kunawapa kiburi wachokozi lakini pia kunadhoofisha sana msingi wa Hati ya Umoja wa Mataifa.”

Vilevile amesema: “Suala la pili ambalo nalo linatia wasiwasi, ni matumizi mabaya ya makusudi ya mamlaka ya Baraza la Usalama kulikofanywa na nchi tatu za Ulaya zilizokuwemo kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Jaribio lao lililoshindwa la kuanzisha utaratibu unaoitwa “snapback” chini ya azimio 2231 (2015), lilikuwa ni hatua isiyo na msingi na haramu kwani imeirejeshea vikwazo Iran ambavyo vilishaondolewa kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *