Umoja wa Mataifa umepinga taarifa ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani aliyedai kiuongo kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa la Kusaidia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) lina uhusiano na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari kwamba: “Tayari tulishalizungumza hili suala huko nyuma. Hakuna uhusiano wowote baina ya UNRWA na Hamas.”

Marco Rubio waziri wa mambo ya nje wa Marekani ametoa madai ya uongo wakati alipotembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu akisema kwamba Umoja wa Mataifa upo katika Ukanda wa Ghaza, lakini UNRWA haitopewa nafasi yoyote na kudai kiuongo kwamba eti UNRWA ni “shirika tanzu la Hamas.”

Farhan Haq ameyasuta madai hayo ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani na kusisitiza kwamba UNRWA ina jukumu muhimu la kibinadamu huko Ghaza.

Amesema: “UNRWA ni uti wa mgongo wa shughuli zetu (sisi Umoja wa Mataifa) za kibinadamu huko Ghaza. Kulikuwa na idadi ndogo ya wafanyakazi wa UNRWA ambao walikuwa na uhusiano na Hamas na tulifuatilia jambo hilo na kuwaondoa watu hao.”

Naibu msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa pia amesema: “Hakuna uhusiano wowote uliopatikana kati ya wafanyakazi wengine kama ambavyo pia hakuna ushahidi wowote uliotolewa wa kuthibitisha madai hayo.”

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iliamua siku ya Jumatano kwamba Israel inalazimika chini ya Mkataba wa Geneva kurahisisha mipango ya kufikishwa ya kibinadamu huko Ghaza kupitia mashirika yasiyoegemea upande wowote kama vile Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na UNRWA, ili kuhakikisha kwamba misaada ya kutosha inawafikia wakazi wa Ukanda wa Ghaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *