
Sudan imekumbwa na moja ya mambo ya dharura mno ya kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na zaidi ya watu milioni 9.6 wakimbizi wa ndani wakiwemo karibu watoto milioni 15.
Katika taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa na Mpango wa Chakula Duniani yametaka hatua za haraka na za dharura zichukuliwe kimataifa kushughulikia mgogoro wa Sudan.
Taarifa ya mashirika hayo ya kimataifa pia imesema: “Ni zaidi ya siku 900 zimepita tangu kuanza mapigano ya kikatili, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, njaa, na kutoweka huduma muhimu katika maisha ya wanadamu mambo ambayo yamewalazimisha mamilioni ya watu kukimbia na kuishi maisha mazito sana hasa wanawake na watoto wadogo.”
Wakati wa ziara za hivi karibuni nchini Sudan, viongozi wakuu kutoka mashirika manne ya Umoja wa Mataifa walishuhudia athari mbaya ya mgogoro kote nchini humo ikiwa ni pamoja na Darfur, Khartoum na maeneo mengine yaliyoathiriwa na migogoro mbalimbali iliyosababishwa na vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF.
Taarifa ya mashirika hayo imeongeza kwa kusema: Sasa vita vya Sudan vimo kwenye mwaka wake wa tatu, mgogoro huo umeharibu huduma muhimu kama vile za afya na elimu. Njaa imeyakumba maeneo mengi ya Sudan na itaendelea kuwa janga kwa wananchi wa nchi hiyo huku watoto wadogo wakiwa miongoni mwa walioathiriwa zaidi.