
Waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni ametamka bayana kwamba utawala huo ambao umefanya jinai kubwa mno za kuchupa mipaka kwa muda wa miaka miwili kwenye Ukanda wa Ghaza, hauwezi kuangamiza mahandaki na njia ya chini ya ardhi za makundi ya Muqawama yakiongozwa na HAMAS.
Televisheni ya Al Jazeera imemnukuu Israel Katz akisema hayo mbele ya naibu rais wa Marekani wakati akiwa safarini mjini Tel Aviv.
Akizungumza na JD Vance, naibu rais wa Marekani, Israel Katz, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni amekiri kwamba zaidi ya asilimia 60 ya mahandaki na njia za chini ya ardhi ziko vilevile kama zamani huko Ghaza na hazijaathiriwa na mashambulizi ya kikatili ya miaka miwili ya Israel.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimekuwa vikitangaza mara kwa mara kwamba ni jambo lisilowezekana kuangamiza mahandaki ya makundi ya Muqawama huko Ghaza kwani mtandao wa mahandaki na njia hizo za chini ya ardhi ni mkubwa na tata mno na Israel haiwezi kabisa kukabiliana nao.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, hakuna uwezekano wowote wa kumaliza mahandaki huko Ghaza na kwamba makundi ya Muqawama yataendelea kutumia njia hizo tata mno za chini ya ardhi kwa ajili ya harakati zao za kuhama sehemu moja hadi nyingine na kwa ajili ya kuwashambulia Wazayuni.
Maafisa wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanakiri kwamba mtandao wa mahandaki umejengwa kwa ustadi na ufundi mkubwa usioelezeka huko Ghaza. Njia hizo hata hazifanani na ni tata mno na kwamba Israel haina taarifa za kutosha kuhusu muundo na idadi ya mahandaki hayo.