Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametaka Umoja wa Mataifa kuwakilisha kwa dhati haki za mataifa yote, huku akilaani uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran na msimamo wa kupendelea upande mmoja wa Baraza la Usalama la umoja huo.

Akihutubia hafla ya kuadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu jijini Tehran, Esmaeil Baghaei amesema kuwa kulinda amani na usalama wa kimataifa, pamoja na kukuza uhusiano wa kirafiki kwa msingi wa usawa wa haki na haki ya kujitawala kwa mataifa, ndizo dhamira kuu za Umoja wa Mataifa.

Baghaei amebainisha masikitiko yake kwamba tangu kuanzishwa kwa Umoja huo, misingi yake imekuwa ikikiukwa, ikitafsiriwa kiholela, na kutumiwa vibaya mara kwa mara na mataifa ambayo bado yana fikra za kikoloni na dhana ya kuwa ubora kuliko mataifa mengine.

Amesema matokeo ya kukiukwa misingi hiyo ni  hali ya sasa ya dunia, iliyojaa vita visivyoisha, dhuluma za kila namna, na utu wa binadamu kudhalilishwa kwa sababu ya tamaa na ubaguzi wa rangi.

Aidha, amekemea vikali “ubabe wa upande mmoja wenye misimamo ya kijeshi” unaoendeshwa na Marekani na washirika wake, ambao umeitumbukiza dunia katika hali ya hatari na machafuko yasiyokuwa na mfano.

Baghaei amesisitiza kuwa bila shaka, Marekani na baadhi ya washirika wake ndio wavunjaji wakuu wa misingi na malengo ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Baghaei, mauaji ya halaiki katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, pamoja na mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Israel dhidi ya mataifa kadhaa, vitendo vya kigaidi, na uvamizi wa maeneo ya mataifa huru , vyote vikiwa na “msaada kamili na ushirikiano” wa Marekani na baadhi ya serikali za Ulaya, ni mambo ambayo yameibua mazingira ya “kutokuwajibika kabisa.”

Mwanadiplomasia huyo wa Iran pia amelaani “vitendo vya uchokozi na vitisho vya mara kwa mara” vya Marekani dhidi ya Venezuela, Cuba, Colombia, Nicaragua, Brazil, na mataifa mengine ya Karibiani na Amerika ya Kusini, akisema kuwa hayo yanakiuka amani na usalama wa kimataifa.

Akiashiria hujuma ya pamoja la Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo mwezi Juni, iliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 1,064 wakiwemo makamanda wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na raia wa kawaida, Baghaei amesisitiza umuhimu wa Iran kuishinikiza jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuwajibika.

Ameongeza kuwa Baraza la Usalama, “kutokana na ushawishi wa Marekani, limeshindwa hata kutoa tamko fupi la kulaani shambulio hilo.”

Licha ya upendeleo ulio wazi ndani ya Baraza la Usalama na taasisi nyingine za Umoja wa Mataifa, pamoja na “maazimio yasiyo halali na ya kionevu” dhidi ya Iran, Baghaei amesema Tehran haijawahi kukiuka Hati ya Umoja wa Mataifa au kudharau misingi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *