HESABU za kocha mpya Mreno wa Yanga Pedro Goncalves, zinaanza leo kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar, wakati mabingwa hao wakiivaa Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Iko hivi; Yanga baada ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika timu ikiongozwa na Patrick Mabedi, miamba hiyo inarejea kuwapa mashabiki wao uhondo kwa upande wa Ligi Kuu Bara na balaa linaanza na Mtibwa Sugar.
Wakati Yanga ikijipambania kimataifa, Mtibwa yenyewe ilikuwa bize kusaka pointi kwa upande wa ligi na mpaka sasa imekusanya tano katika mechi nne ikishinda moja, sare mbili na kupoteza moja.
Yanga inaingia uwanjani leo ikiwa tayari imecheza mechi mbili za ligi msimu huu na kukusanya pointi nne kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji na matokeo ya 0-0 dhidi ya Mbeya City.
Rekodi zinaonyesha katika mechi kumi za Ligi Kuu zilizopita dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga imeshinda tisa na sare moja. Mara ya mwisho Yanga kupoteza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ilikuwa Aprili 17, 2019. Katika ushindi wa mechi hizo tisa, nane ni mfululizo.
Licha ya uimara wa Yanga, ni wazi safu ya ulinzi ya Mtibwa ni ngumu kufunguka kwani imeruhusu bao moja tu katika mechi nne ilizocheza msimu huu ikirejea Ligi Kuu Bara.
BENCHI LA UFUNDI
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema kocha mkuu mpya wa kikosi hicho Pedro na msaidizi wake Felipe Pedro wanaanza kazi rasmi leo dhidi ya Mtibwa.
Kamwe amesema Patrick Mabedi ambaye aliiongoza timu akiwa Kaimu Kocha Mkuu kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers na kufuzu makundi baada ya kuondoka kwa Romain Folz, sasa atakuwa msaidizi namba mbili.
“Kesho (leo) Mungu akipenda kocha mkuu atakuwa uwanjani tayari kwa kazi, kwani tumebakiza vitu vichache tu kukamilisha masuala ya kiutaratibu.
“Tunafanya jitihada zote ili kocha Pedro aweze kukamilisha masuala ya kikanuni na sheria ili aweze kuwa sehemu ya mchezo huu.
“Mchezo wa mwisho wa ligi hatukumaliza vyema na kila mtu aliona mchango wa mchezaji wa 12 (mashabiki) dhidi ya Silver, hivyo tutarajie mazuri kesho (leo),” amesema Kamwe.
Mbali na Filipe, ambaye ni kocha msaidizi wa kwanza, kocha Pedro pia amekuja na kocha wa makipa, Fernando Pereira ambaye atachukua nafasi ya Majdi Mnasria.
Goncalves pia amebakiziwa kocha wa viungo Tshephang Mokaila raia wa Botswana ambaye mabosi wa Yanga walipambana kumbakisha kwenye kikosi hicho kufuatia kuvutiwa na ujuzi wake.
MZIZE OUT, ECUA FRESHI
Kamwe amesema: “Mzize (Clement) alijitonesha, hivyo bado hayuko sawa na mpaka baadae tutajua kama yupo au la, Ecua (Celestine) pia yuko salama, yuko nje tu kwa maswala ya kiufundi.
“Kama mechi ya kesho (leo) itamuhitaji basi kocha atampanga na mashabiki watamuona tena kwani jamaa yuko vizuri kwa ajili ya kazi.”