
Rais Masoud Pezeshkian amesisitiza historia ya muda mrefu na yenye upendo ya uhusiano kati ya Iran na Oman na kusema: “Mawasiliano na maingiliano kati yao yamekuwa yakiegemezwa katika misingi ya udugu, kuheshimiana na nia njema, na nchi hizo mbili daima zimekuwa ni wasaidizi na waungaji mkono wa kila mmoja katika hali ya misukosuko ya kieneo.”
Rais Pezeshkian amesema hhayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Hamoud bin Faisal al Busaidi Waziri wa Mambo ya Ndani wa Oman ambapo sambamba na kusifu nafasi ya kiujenzi ya Oman katika medani za kieneo ameongeza kuwa: Juhudi za Oman katika kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika uga wa upatanishi na kuandaa mazungumzo kati ya Tehran na Washington zinastahiki kupongezwa na zinaonyesha utendaji wa hekima na wa kutafuta amani wa viongozi wa nchi hiyo.
Rais wa Iran ameashiria pia msimamo wa wazi na usio na shaka wa Oman katika kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Gaza na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni, na akasema: “Msimamo huu wa kibinadamu na Kiislamu wa Oman ni wa thamani kubwa. Sisi Waislamu, tunathamini huruma na uungaji mkono huu, na lau nchi zote za Kiislamu zingewaunga mkono watu wa Gaza kwa utendaji huu, basi tusingeshuhudia matukio ya uchungu na ya kusikitisha katika eneo hili.”
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Rais Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa umoja wa Umma wa Kiislamu na kusema: “Sisi Waislamu, kwa kuzingatia mafundisho ya kidini na nasaha za Mtukufu Mtume (SAW), ni ndugu baina yetu na tunapaswa kusimama kidete. Tukifanyia kazi mafundisho haya, Umma wa Kiislamu utakuwa na nguvu kubwa itakayodhamini maslahi ya mataifa ya Kiislamu na usalama wao na kuzuia kuvamiwa nchi za Kiislamu.