Balozi wa China nchini Iran amesema kuwa nchi yake haitosita kuchukua hatua za kukabiliana na vikwazo dhidi ya Iran ikiwa vikwazo hivyo vitaathiri maslahi yake na kukwamisha shughuli na uhusiano wake wa kibiashara na Tehran.

Cong Peiwu alisema hayo jana Jumatatu mbele ya waandishi wa habari hapa jijini Tehran na kuongeza kwamba China haitasita kuchukua hatua ikiwa maslahi yake ya kiuchumi yataathiriwa na vikwazo vilivyowekwa kwenye sekta ya biashara ya Iran. Cong ametoa matamshi hayo akijibu maswali kuhusu jinsi China inavyofuatilia vikwazo vya hivi karibuni vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, ambavyo vilirejeshwa mwishoni mwa Septemba baada ya nchi za Ulaya zilizokuwemo kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuyavuruga kwa makusudi mapatano hayo na kudai kuwa Tehran haikuyaheshimu. 

Lakini Iran, Russia na China zinaamini kwamba hatua ya nchi za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kurudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran ni kinyume cha sheria ndio maana nchi mbili za Russia na China hazitambui vikwazo hivyo hata kama Umoja wa Mataifa umevipasisha chini ya mashinikizo ya nchi za Magharibi. Balozi wa China mjini Tehran ameongeza kuwa, Beijing itaendelea kuwa na ushirikiano wa karibu na Tehran na kusisitiza kwamba Iran na China zina msimamo mmoja wa kupinga siasa za nyuso mbili duniani. China ni mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Tehran na ndiye mnunuaji mkubwa wa mafuta ya Iran.

Kwa mujibu wa Press TV, tathmini zinaonesha kuwa, zaidi ya 92% ya mauzo ya nje ya mafuta ya Iran huishia nchini China, licha ya vikwazo vikali vilivyowekwa na Marekani kwa kila anayenunua mafuta ya Iran. Wataalamu wanaamini kuwa China inategemea sana mafuta ya Iran hasa kutokana na wepesi wa kuyapata tena kwa bei nafuu ambayo inasaidia sana ustawi wa sekta yake ya viwanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *