Dar es Salaam. Katika nchi inayoelekea kuwa ya maarifa, maendeleo ya kweli hayawezi kufikiwa bila kukuza utamaduni wa kusoma. Kusoma si jambo la anasa tena, bali ni hitaji la msingi kama ilivyo afya, elimu na miundombinu.

 Katika muktadha huu, Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (Bohumata) ni chombo mama, mhimili mkuu wa maendeleo ya usomaji nchini. Hata hivyo, hali ilivyo sasa inaashiria kwamba bodi hii imezama katika usingizi wa pono.

 Wakati ni sasa wa kuchukua hatua madhubuti, kuimarisha maktaba za umma, binafsi na zile za shule kwa lengo moja kuu la kukuza utamaduni wa kusoma kwa Watanzania wote.

Hakuna jamii yoyote iliyoendelea duniani bila kuweka mkazo katika usomaji. Maktaba ni chemichemi ya maarifa; ni sehemu ya kukuza fikra, kutunza historia na kuchochea ubunifu. 

Maktaba si tu jengo lenye vitabu, bali ni mahali pa kutengeneza ndoto na kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushindana duniani. Kwa bahati mbaya, kwa miaka mingi, sekta hii muhimu imeachwa kwenye kona ya giza, na Bodi imeonekana kulegalega katika kutimiza wajibu wake.

Bodi ya Huduma za Maktaba ni chombo kilichoundwa mahsusi kuendesha, kusimamia na kuendeleza huduma za maktaba nchini. Ilitarajiwa iwe kiini cha mapinduzi ya maarifa, kinara wa sera bora na msukumo wa mabadiliko chanya katika sekta ya usomaji.

 Lakini leo hii, tunaona maktaba zikiwekwa kando kama vitu visivyo na umuhimu. Je, bodi haioni kwamba taifa lisilo na utamaduni wa kusoma ni taifa lisilo na dira? Je, bodi haijitambui kuwa imebeba dhamana kubwa ya kiutamaduni na kielimu? Lazima tujiulize: Bodi ipo kwa ajili ya nani ikiwa si kwa Watanzania wanaotaka kusoma?

Ni jambo la kusikitisha kwamba kila baada ya hatua chache katika miji na vijiji vyetu tunaona baa, vibanda vya pombe na maeneo ya starehe. Lakini ni nadra tena sana kukutana na maktaba ya umma, au hata ya binafsi.

 Hii ni ishara ya wazi kuwa kama taifa tumepoteza mwelekeo. Lakini zaidi ya hapo, ni onyesho la uzembe wa Bodi. Kama bodi ingeweka mikakati madhubuti, tungekuwa tunaona utitiri wa maktaba badala ya baa. Tunahitaji mabadiliko ya dhati; mabadiliko ya sera, mtazamo na utekelezaji.

Uimarishaji maktaba

Ni lazima maktaba za umma zipewe kipaumbele. Hizi ndizo zinazoweza kuwafikia wananchi wa kawaida, watoto wa familia zisizo na uwezo wa kununua vitabu, na vijana wanaotafuta maarifa nje ya mfumo rasmi wa elimu. Lakini hali ilivyo sasa, maktaba hizi ni chache, nyingi hazina vitabu vya kisasa,  na mazingira yake hayavutii.

Watoto wa shule ndio mustakabali wa taifa. Ikiwa tutashindwa kuwajengea mazingira rafiki ya kusoma, basi tunalea taifa la kutojua kusoma wala kuandika vizuri. 

Maktaba nyingi za shule ni majina tu; ni vyumba vilivyojaa vumbi na vitabu vilivyozeeka. Hii si haki kwa watoto wetu. Bodi inapaswa kushirikiana na wizara mama kuhakikisha kila shule ina maktaba bora, zenye vitabu vya kuvutia na vinavyolingana na umri wa wanafunzi.

Kwa upande wa sekta binafsi, bodi inapaswa kutoa motisha na kushirikiana na wawekezaji binafsi wanaotaka kuanzisha maktaba. Kama kuna vikwazo vyovyote vya kisera, sheria na vinginevyo, ni wakati sasa Bodi izibe pengo lililopo la sekta binafsi kutojihimu kwenye ujenzi wa maktaba.

Mabadiliko muhimu

Bodi haiwezi tena kukaa kimya, haiwezi kuendelea kulala usingizi wa pono huku taifa likizama kwenye giza la kutojua kusoma.

Hivi majuzi nimesoma uchambuzi wa elimu na hali ya kujua kusoma na kuandika kwa wananchi wa Tanzania Bara uliotolewa Mei 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Wananchi wanaojua stadi hizo ni asilimia chini ya 85.Najiuliza kwa nini tusiwe na asilimia 100, Kwa nini tusifike kule tulipofika miaka ya nyuma mpaka Taifa likatambuliwa na Unesco?

 Kuna haja ya mapinduzi ya usomaji, na mapinduzi haya hayawezi kufanikiwa bila Bodi kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu. Tunahitaji sera mpya zinazoweka kipaumbele kwenye ujenzi na uboreshaji wa maktaba, mikakati ya ufadhili wa maktaba kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na  mafunzo kwa wasimamizi wa maktaba kote nchini.

Pia, tunahitaji kampeni za kitaifa za kukuza usomaji, zikihusisha vyombo vya habari na shule, teknolojia ya kisasa kuingia katika maktaba,vitabu vya kimtandao, ufuatiliaji na tathmini ya maktaba zilizopo ili kuzifufua.

Watanzania wako tayari

Ukweli ni kwamba kuna kiu ya maarifa miongoni mwa Watanzania. Vijana wanatafuta maarifa, wazazi wanataka watoto wao wasome, walimu wanahitaji rasilimali bora. Lakini wapi pa kwenda? Bodi ni kama baba wa familia aliyeshindwa kujenga nyumba salama kwa watoto wake. Ni wakati sasa wa kuchukua hatua  sio kwa kauli tu, bali kwa vitendo, hasa kwa kuzingatia uongozi thabiti wa Bodi uliopo sasa na maono yake.

Bodi lazima ibadilike.  Sio kwa sababu ni shinikizo, bali kwa sababu ni wajibu wake wa msingi. Tumechoka kuona baa kila kona, wakati watoto wetu hawana sehemu ya kusoma. Tunahitaji mabadiliko.

Tunataka maktaba zenye vitabu vya maana, maktaba zenye mazingira rafiki, maktaba ambazo ni kitovu cha jamii.

Watanzania hawahitaji miujiza, wanahitaji majibu. Na jibu kubwa zaidi linapatikana katika kurudisha heshima ya maktaba. Hili haliwezekani kama Bodi itaendelea kulala. 

Ni wakati wa kuamka, kuchukua hatua, na kutuonesha kwamba bado ina uwezo wa kuongoza mapinduzi ya kusoma nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *