Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Bi. Rugwabiza amesema maandalizi ya uchaguzi huo wa urais, wabunge, serikali za mitaa na mikoa yamepiga hatua kubwa, lakini bado bajeti ya maandalizi inakabiliwa na pungufu ya takribani dola milioni 12.
Valentine Rugwabiza, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mkuu wa MINUSCA akihutubia katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali nchini humo.
“Serikali ya CAR imeonesha dhamira ya kweli ya kisiasa kwa kuongeza dola milioni 7.8 katika Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaoratibu maandalizi ya uchaguzi kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP,” amesema Bi. Rugwabiza wakati wa hotuba hiyo ya kuwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali ya CAR kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
“Hata hivyo, tunatoa wito kwa washirika wote kuongeza msaada wao ili uchaguzi huu uwe wa kuaminika, salama na wa wakati.”
Idadi ya wanawake wapiga kura yaongezeka, wapiganaji wajisalimisha
Bi. Rugwabiza ameeleza kuwa zaidi ya wapiga kura milioni 2.3 wamesajiliwa, ambapo asilimia 47.2 ni wanawake, jambo linaloashiria ushirikishwaji mkubwa wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.
Katika taarifa yake, amepongeza serikali ya Rais Faustin Archange Touadéra kwa kuendeleza juhudi za amani kupitia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini tarehe 19 Aprili 2025, kati ya serikali na makundi mawili makubwa ya waasi – UPC na 3R.
MINUSCA imekuwa ikisaidia mipango ya upokonyaji silaha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
Hatua hiyo imechochea ufanisi wa operesheni za wapiganaji kupokonywa na kusalimisha silaha na kujumuishwa kwenye jamii au (DDRR) ambapo zaidi ya wapiganaji 700 wameachia silaha zao tangu Julai mwaka huu.
Bado hali ni tete mipakani
Pamoja na mafanikio hayo, Bi. Rugwabiza ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, (MINUSCA), ameonya kuwa hali ya usalama inasalia tete katika maeneo ya mpakani na Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hususan katika majimbo ya Haut-Mbomou na Vakaga, kutokana na uvamizi wa makundi yenye silaha na mapigano yanayoendelea katika nchi jirani.
Ukata kuleta changamoto kwenye operesheni
Amesisitiza kuwa MINUSCA itaendelea kulinda raia na kusaidia utoaji wa misaada ya kibinadamu, ingawa operesheni zake zinakabiliwa na changamoto za kifedha.
“Tumeagizwa kupunguza matumizi kwa asilimia 15 katika mwaka wa fedha 2025/2026, jambo linaloweza kuathiri vibaya utekelezaji wa majukumu muhimu kama ulinzi wa raia, mchakato wa uchaguzi na juhudi za amani,” ameonya.
Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
Chonde chonde ongezeni muda wa MINUSCA
Katika hitimisho lake, Bi. Rugwabiza amelisihi Baraza la Usalama kuongeza muda wa mamlaka ya MINUSCA kwa mwaka mmoja zaidi kwa kiwango chake cha sasa cha watumishi, akisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa uthabiti wa kisiasa na kiusalama wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na ukanda mzima wa Afrika ya Kati.
“Miezi michache ijayo itakuwa ya maamuzi. Tunahitaji mshikamano wa kimataifa ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana katika amani na usalama hayapotei,” amesisitiza.
Kwa sasa, jumla ya makundi 11 kati ya 14 yaliyokuwa yamesaini makubaliano ya kisiasa yamejitangaza rasmi kuvunjika, ishara ya matumaini mapya kwa safari ya kudumu ya amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.