
Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake leo Jumanne Oktoba 28, Katibu Mkuu pamoja na kupokea ripoti za kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, amepokea kwa masikitiko taarifa za matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa vyombo vya usalama na vurugu zilizotokea kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama.
Vyombo vya habari vinaripoti kwamba Mahakama ya Juu nchini Cameroon ilitangaza Jumatatu kuwa Rais wa sasa, Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92 ameshinda uchaguzi wa Rais, ikiwa ni baada ya siku kadhaa za makabiliano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa vyama vya upinzani waliokuwa wanadai matokeo halali. Katika vurugu hizo yaripotiwa watu wanne walipoteza maisha.
Guterres ameeleza huzuni yake kutokana na vifo vilivyotokea pamoja na taarifa za kuweko kwa majeruhi yaliyotokea, na ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathiriwa wa tukio hilo.
Katibu Mkuu ameitaka serikali ya Cameroon kufanya uchunguzi wa kina na huru kuhusu matukio hayo, ili kuwawajibisha wote watakaopatikana na makosa.
Pande zote zijizuie kutumia nguvu na kauli za chuki
Aidha, amewataka wadau wote wa kisiasa na wafuasi wao kujizuia kutumia nguvu, kuepuka kauli za uchochezi na hotuba za chuki ambazo zinaweza kuongeza mgawanyiko nchini humo.
“Tunahimiza umuhimu wa kulinda haki za binadamu na uhuru wa msingi wa raia wote,” amesema Katibu Mkuu, akisisitiza kuwa mamlaka zinapaswa kuhakikisha mazingira salama na yenye amani, pamoja na kuheshimu taratibu za kisheria kwa wale wote waliokamatwa.
Vilevile, ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa yenye ushirikishwaji mpana ili kushughulikia malalamiko yaliyopo, kulinda umoja wa kitaifa na kudumisha uthabiti wa nchi hiyo.
Paul Biya amekuwa anaongoza Cameroon, taifa hilo lililoko Afrika ya Kati tangu mwaka 1982.