Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Tessa Wong
- Nafasi, BBC Reporter
-
China imezindua idadi kubwa ya silaha mpya, ndege zisizo na rubani na vifaa vingine vya kijeshi katika gwaride kubwa ambalo waangalizi wengi wanaona kuwa ni ujumbe wa wazi kwa Marekani na washirika wake.
Katika hafla hiyo, Rais Xi Jinping aliwakaribisha zaidi ya wakuu 20 wa nchi za kigeni, akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, ambao wote wanaitegemea China kwa msaada wa kiuchumi na mwingine.
Gwaride hilo lilikuwa ni onyesho la kuimarika kwa uwezo wa Bwana Xi duniani, pamoja na uwezo wa kijeshi wa China, na ulikuwa na kombora la “Guam Killer”, ndege isiyo na rubani ya “Loyal Companion” na hata mbwa mwitu wa roboti.
Lakini zaidi ya vishindo na silaha mpya, tulijifunza nini kutokana na sherehe hiyo?
Yafuatayo ni mambo makuu matano
1. China ina silaha nyingi, lakini ni kiasi gani inaweza kuzitumia?
Gwaride la Jumatano lilionyesha kuwa China imeweza kuzalisha viwango mbalimbali vya silaha kwa muda mfupi.
Michael Raska, profesa msaidizi katika Mpango wa Maendeleo ya Kijeshi katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nanyang cha Singapore, anabainisha kwamba miaka kumi iliyopita, teknolojia ya kijeshi ambayo China ilionyesha ilihusisha zaidi “nakala za msingi” za vifaa vya hali ya juu zaidi ambavyo Marekani ilikuwa imetengeneza.
Lakini gwaride hili lilionyesha uvumbuzi mpana zaidi na aina mbalimbali za silaha, hasa ndege zisizo na rubani na makombora, ambayo yanaonyesha kiwango cha maendeleo ya Kichina katika ulinzi na viwanda.
Alexander Neil, mwenzake katika Jumuiya ya Pasifiki, anabainisha kuwa muundo wa serikali kuu ya China, unaotoka juu chini na rasilimali muhimu umeiwezesha kuzalisha silaha kwa kasi na kiwango ambacho nchi nyingi haziwezi kufanya.
Uwezo huu wa uzalishaji mkubwa kwenye uwanja wa vita unaweza kuipa China faida na kumshangaza mpinzani kwa idadi.
“China ina uwezo wa kuzalisha kwa wingi risasi, meli, vifaa hivi vyote,” anasema Bw. Neill. “Serikali inaweza kutoa maagizo ya uzalishaji na kila kitu kinaendelea.” Lakini ni kwa kiwango gani jeshi la China linaweza kuendesha mifumo hii ya silaha bila kizuizi?
“China inaweza kuonyesha kifaa hiki cha hali ya juu, lakini ina uwezo wa kukitumia?” anauliza Dr. Raska.
Anaamini hili halitakuwa rahisi kwa sababu jeshi la China ni kubwa sana na halijajaribiwa, na halijahusika katika vita vyovyote vikubwa kwa miongo kadhaa.
2. China inashughulikia silaha zake za makombora ili kuikabili Marekani
Gwaride hilo lilikuwa na aina mbalimbali za makombora, ikiwa ni pamoja na aina mpya, ikiwemo kombora la Dongfeng-61 lenye uwezo wa kubeba vichwa vingi vya nyuklia, kombora la masafa marefu la Dongfeng-5C lenye masafa yanayoweza kufika Marekani kutoka kaskazini mwa China, na kombora la masafa ya kati la Dongfeng-26D, linalojulikana kama “Guam Killer” ambalo linaweza kulenga kambi muhimu ya kijeshi ya Marekani ya Guam.
Chanzo cha picha, Getty Images
Makombora kadhaa ya supersoni ya kukabiliana na meli za kivita, kama vile YG-17 na YG-19, yalionyeshwa pia, ambayo yameundwa kwa kasi ya juu na ujanja wa kupita mifumo ya kuzuia kombora.
Kuna sababu ya kuzingatia idadi hi ya makombora.
Bw. Neil anasema China inatengeneza makombora na vikosi vya makombora kama sehemu kuu ya mkakati wake wa kuzuia na kukabiliana na ubora wa jeshi la majini la Marekani.
Jeshi la Wanamaji la Marekani halina mpinzani duniani kwa kundi lake kubwa la meli za kivita za kubeba ndege, ilhali China bado iko nyuma katika eneo hili.
Lakini Bw. Neil anadokeza kwamba baadhi ya vyanzo katika jumuiya ya ulinzi ya Magharibi vinazidi kubishana kuwa vikundi hivi vya mashambulizi viko hatarini kwa sababu ni shabaha rahisi kwa shambulio lolote la kombora.
Anasema Beijing sio tu inaimarisha uzuiaji wake lakini pia inakuza “uwezo wa shambulio la pili,” uwezo wa kulipiza kisasi katika tukio la shambulio la kigeni.
Silaha zingine zinazojulikana ni pamoja na silaha ya leza ya LY-1 inayojadiliwa sana, ambayo kimsingi ni leza kubwa inayoweza kuteketeza au kuzima vifaa vya kielektroniki au hata kuwafanya marubani kuwa vipofu.
Msururu wa ndege za kivita za siri za kizazi cha tano, zikiwemo J-20 na J-35, pia zilionyeshwa.
3. China inafanya vyema katika nyanja ya akili bandia na ndege zisizo na rubani
Ndege mbalimbali zisizo na rubani zilionyeshwa, baadhi zikiwa na akili ya bandia, lakini ndege kubwa isiyo na rubani ya chini ya maji, GX-002, ilivutia watu wengi zaidi.
Ndege isiyo na rubani, inayojulikana pia kama “Gari Kubwa Sana la Chini ya Maji Isiyo na Rumani,” ina urefu wa hadi mita 20 (futi 65) na inaweza kufanya kazi za uchunguzi na upelelezi.
Chanzo cha picha, Getty Images
China pia ilionyesha ndege yake isiyo na rubani, JG-11, iliyopewa jina la “Loyal,” ambayo inaweza kuruka pamoja na ndege ya kivita iliyo na mtu na kuisaidia katika mashambulizi.
Mbali na ndege zisizo na rubani za kawaida, “mbwa mwitu wa roboti” pia walionyeshwa. Wataalamu wanasema roboti hizi zinaweza kutumika kwa kazi mbalimbali, kuanzia kugundua na kusafisha migodi hadi kuwafukuza wanajeshi wa adui.
Maonyesho hayo ya ndege zisizo na rubani yanaonyesha mwelekeo wa wazi ambao China inataka kuchukua na mkakati wake wa kijeshi, ambao “sio tu kuimarisha miundo ya kijeshi ya jadi, lakini kuchukua nafasi yao.”
Dk. Raska anabainisha kuwa China imejifunza wazi kutokana na vita vya Ukraine kwamba inatosha “kurusha ndege zisizo na rubani kwa adui” ili kudhoofisha ulinzi wake.
“Kasi ni muhimu katika msururu wa mauaji,” anasema Bw. Neil, akibainisha kwamba katika vita vya haraka, maamuzi lazima yafanywe kwa “sekunde zilizogawanyika” ili kumshinda adui na kuwa kifua mbele, jambo ambalo AI inaweza kufanya.
Anaongeza kuwa nchi nyingi bado zinasitasita kuhusu AI katika mifumo yao ya kijeshi, akiuliza, “Je, tunastarehe gani kuweka AI katika msurur wa mauaji?”
Dk. Raska anasema China inafurahishwa sana na hili: “China inaamini inaweza kutumia AI. Wamedhamiria kuijumuisha kikamilifu katika mifumo yao.
4. China inaweza kuwa na teknolojia, lakini Marekani bado ina fursa ya uendeshaji
Gwaride hilo lilionyesha wazi kuwa China inaikaribia Marekani kwa kasi katika teknolojia ya kijeshi na ina rasilimali za kujenga silaha nyingi.
Lakini wataalam wanasema Marekani bado inadumisha ubora wake wa kiutendaji.
Dk. Raska anabainisha kuwa jeshi la Marekani limepiga hatua” kwa sababu ya utamaduni wa “chini-juu” ambapo vitengo vya ardhini vinaweza kufanya maamuzi na kubadilisha mikakati yao ya mapigano kadiri hali inavyobadilika, na kuwapa wepesi wakati wa mapigano.
Kwa maoni yake, jeshi la China lina muundo wa “juu-chini” na, hata kwa mifumo ya hali ya juu, haitasonga bila maagizo kutoka kwa viongozi wa juu.
Dk. Raska anataja matukio ya hivi majuzi, kama vile tukio la mwezi uliopita wakati meli ya kivita ya Uchina ilipogonga moja ya meli ndogo wakati wa makabiliano kati ya meli za kijeshi za China na Ufilipino: “Wachina wanafikiri teknolojia yao inatoa kizuizi na hiyo inatosha kwa Marekani, lakini kiutendaji, kuna ushahidi kwamba hawana nguvu kama wanavyodai.”
5. Gwaride la China lilikuwa fursa ya kutangaza silaha na pia kuonyesha msimamo wa pamoja kwa Marekani
Bw. Neil anabainisha kuwa kwa kuwaalika viongozi kutoka nchi kadhaa kwenye hafla hiyo, gwaride la kijeshi la China lilikuwa jambo kubwa la kutangaza kuuza silaha kwa wateja watarajiwa.
Baadhi ya nchi, kama vile Myanmar, ni wanunuzi wa kawaida wa silaha za China, lakini Dk. Raska anabainisha kuwa fursa ya kuwauzia wateja wapya au kuongeza oda ni njia ya serikali ya China kupanua ushawishi wake duniani.
Miongoni mwa wateja wakuu ni wale waliokuwepo pamoja na Xi Jinping, Vladimir Putin na Kim Jong-un.
Watatu hao, ambao walitembea pamoja hadi kwenye uwanja wa gwaride na kusimama kwenye jukwaa, waliwasilisha mbele umoja wao.
Bw. Neill anasema huu ulikuwa ujumbe kwa Marekani: ikiwa Marekani ilitaka kuwapa changamoto, ingelazimika “kupigana nao wakati huo huo katika nyanja nyingi zinazowezekana: Rasi ya Korea, Mlango-Bahari wa Taiwan na Ukraine.”
“Ikiwa utazingatia hilo, kuweka shinikizo kwa Marekani katika maeneo yote matatu kunaweza kusababisha kushindwa katika mojawapo ya maeneo haya,” anaongeza