Picha, inayoripotiwa kuchukuliwa na kuchapishwa na mwanajeshi wa Israel, imesababisha mshtuko mkubwa katika mitandao ya kijamii, ikithibitisha ripoti za jinsi utawala huo vamizi unavyowatumia wazee wa Palestina kama ngao za binadamu katika vita vya muda mrefu vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Picha hiyo, iliyosambazwa sana na akaunti ya “Israel Genocide Tracker”, ambayo inarekodi uhalifu wa kivita wa Israel, inaonyesha wanaume wawili wazee wa Kipalestina wakiwa wamefungwa mikono na kuvuliwa nguo, huku wakilazimishwa kuingia katika jengo lililoharibika na vita huko Gaza.
“Picha zilizowasilishwa na marafiki wa wanajeshi wa Israel zinakiri kwamba wanajeshi hao waliwatumia Wapalestina waliotekwa nyara, wengi wao wakiwa wazee, kama ngao za binadamu kila siku,” imeandika Israel Genocide Tracker, akaunti ya X inayochanganua mitandao ya kijamii na kukusanya data kuhusu wanajeshi wa Israel.
“Walipojeruhiwa au kuchoka, Wapalestina hao waliagizwa kuingia katika maeneo yaliyotengwa ya mauaji ili wapigwe risasi na askari wengine.”

Picha hiyo inaonyesha wazi kwamba ilinaswa na mwanajeshi wa Israel, ikitoa ushahidi wa moja kwa moja kwa ripoti kwamba Wapalestina wazee hutumika kama ngao za binadamu — uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa.
Picha za baadaye zilionyesha kwamba wanaume hao, ambao wametambuliwa, walipigwa risasi na kuuawa kwa mujibu wa sera ya utawala wa Kiyuni wa Israel kwamba mateka wa Kipalestina waliowatumia kama ngao za binadamu wanapaswa kuuawa mara tu wanapodhoofika sana au kujeruhiwa kiasi kwamba hawawezi tena kutimiza malengo ya watekaji nyara wao.
Tangu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano Oktoba 11, Israel imekuwa ikishambulia Ukanda wa Gaza mara kwa mara kinyume na makubaliano hayo.