Zaidi ya wagonjwa 460 na watu walioandamana nao wameripotiwa kupatikana wameuawa katika hospitali ya uzazi huku kukiwa na ripoti za kuendelea ukatili dhidi ya raia huko El Fasher, Sudan. Hayo yameripotiwa huku mawaziri wa Mambo ya Nje wa Sudan na Misri wakikutana kujadiliana hali ya eneo hilo la magharibi mwa Sudan.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema katika taarifa yake ya jana kwamba, uchunguzi wa picha za satelaiti umeonesha kupatikana ushahidi mpya wa kuendelea mauaji ya umati huko El Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini. Mauaji hayo yalifanyika katika kipindi cha saa 48 tangu kundi la Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF lilipoutwaa mji huo Jumapili wiki hii.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kuweko mashambulizi 185 dhidi ya maeneo ya huduma za afya nchini Sudan. Wafanyakazi wa masuala ya afya 1,204 wameshauawa na wengine 416 kujeruhiwa tangu vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vilipoanza nchini Sudan mwezi Aprili 2023. Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti kwamba zaidi ya watu 36,000 wamekimbia mji wa El Fasher katika kipindi cha baina ya siku Jumapili hadi juzi Jumanne. Shirika hilo limezinukuu duru za ndani zikiripoti kwamba kutokana na ukosefu wa usalama na ukosefu wa njia za usafiri, maelfu ya watu bado wamekwama na hawawezi kukimbia kutoka mjini humo.

Wakati huo huo, jana Jumatano Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty alikutana na waziri mwenzake wa Sudan, Mohieldin Salim na kujadiliana hali ngumu ya kibinadamu na kiusalama katika mji huo wa El Fasher ya Sudan ambao ulitekwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) Jumapili wiki hii. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Cairo, Abdelatty amethibitisha uungaji mkono kamili wa Misri kwa wananchi wa Sudan na kujitolea kwake katika juhudi za kuleta utulivu na amani nchini humo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *