
Mamlaka mjini Mombasa yamewakamata watu 27, wakiwemo watoto 20, wanaoshukiwa kuhusika katika shughuli kama za kidini zinazohusiana na kanisa. Kundi hilo lilikamatwa huko Changamwe kufuatia ripoti ya umma ya watoto waliokuwa wakishikiliwa katika mazingira mabaya na inadaiwa walikuwa wawakikabiliwa na njaa.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Changamwe, Gogo Patrick, amethibitisha kukamatwa kwa watu hao, akisema kwamba maafisa waliingilia kati baada ya kupokea taarifa kuhusu watoto waliokuwa katika hali mbaya ndani ya kanisa la Zion Fire Ministries.
Walipofika, maafisa waliwakuta wanawake saba na watoto 20—wenye umri kati ya miaka miwili na 15—wakiwa wamelala sakafuni, wamefunikwa na blanketi. Patrick ameelezea tukio hilo kama “la kuhuzunisha,” akibainisha kuwa watoto hao walionekana kuwa na utapiamlo na walikuwa wakiishi katika mazingira yasio safi, yaliyojaa mbu.
“Hali ambayo tuliwapata wanawake na watoto ilikuwa ya kuhuzunisha. Walikuwa wamelala sakafuni wazi, wamefunikwa na blanketi pekee, katika eneo lililojaa mbu. Ilikuwa hatari dhahiri kwa maisha yao,” Patrick amesema, kulingana na vyombo vya habari vya Kenya.
Wachunguzi wanaamini kundi hilo lilikuwa likikaa ndani ya kanisa, baada ya kupata mizigo na mali za kibinafsi katika eneo la tukio. Polisi wanasema operesheni hiyo ilifuatia kukamatwa kwa mwanamke siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, ambaye aliwaongoza maafisa wa polisi hadi eneo hilo.
Patrick pia amesema kwamba watoto—wengi wao wakiwa na umri wa kwenda shule—hawakuwepo madarasani wakati mitihani ya kitaifa ikiendelea.
“Leo ni siku ya shule, na mitihani inafanyika kwa sasa. Hata hivyo, watoto kati ya umri wa miaka miwili na 15 walikuwa hapa badala ya kuwa shuleni,” ameongeza. Mamlaka kwa sasa inamtafuta mwanamke anayeaminika kuwa kiongozi au mmiliki wa kanisa hilo, huku uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuwa na msimamo mkali wa kidini ukiendelea. Matukio haya yanakuja huku umakini wa kitaifa ukiendelea kulenga matokeo ya mauaji ya Shakahola. Wakati huo huo, wachunguzi wa mauaji wamerudisha miili 10 zaidi kwa familia, na kufanya jumla ya miili iliyorejeshwa kuwa 11. Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inasaidia familia katika kupanga usafiri wa miili hiyo hadi katika kaunti zao kwa ajili mazishi.
Ndugu wa mmoja wa watu waliofariki, akizungumza baada ya kupokea miili ya wanafamilia wake, alionyesha faraja kwamba mchakato huo hatimaye umeanza.
“Tunashukuru. Tumewaokoa wapendwa wetu wawili na sasa tutapanga mazishi ili kuwazika nyumbani,” amesema.