Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ametangaza kwamba vita vya hivi karibuni vya siku 12 vimefichua uadui unaoendelea wa Marekani, akisisitiza kwamba ingawa mbinu zake zimebadilika, lakini lengo lake la msingi la kupinga Iran yenye nguvu na huru bado halijabadilika.

Akizungumza katika sherehe ya kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa leo Jumanne, Qalibaf ameashiria umuhimu wa kihistoria wa 13 Aban (Novemba 4) katika historia ya sasa ya Iran, akiihusisha na mapambano ya kudumu ya taifa dhidi ya tawala za kigeni.

Qalibaf amesisitiza kwamba kiini cha mfumo wa utawala wa kiimla bado kina mizizi katika “usaliti na udhibiti,” akiikosoa Marekani kwa kuendeleza fikra yake ya uadui chini ya pazia jipya.

Amesisitiza kwamba leo tunashuhudia kwamba asili ya mfumo wa kibeberu haijabadilika na kuusema: “Fikra ile ile iliyokuwepo katika utawala wa Carter dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo ilimlinda na kumuunga mkono Shah mlaaniwa, iliyohusika katika kula njama, bado ipo hii leo kwa roho ile ile yenye zana za kisasa zaidi kuhusu Iran.”

Spika wa Bunge la Iran ameendelea kusema: “Leo, na kwa mtazamo uleule wa kibeberu, wanawaua wanasayansi wetu mjini Tehran, katikati ya Iran. Wanaona ni haki yao kwamba Iran haipaswi kuwa na nguvu, na hata ikiwa ni hivyo, haipaswi kuwa huru.”

Qalibaf ameongeza kwamba maadui “wanataka kuficha sura zao za uhalifu kwa kutumia maneno kama ‘shambulio la kuzuia,’ lakini ukweli ni kwamba wanapinga Iran huru na iliyoungana.”

Spika Qalibaf amesema: “Msingi wa 13 Aban ni mapambano ya taifa la Iran dhidi ya utawala na kibeberu,” na kusisitiza kwamba kanuni hii inasalia kuwa msingi wa sera ya kigeni ya Iran, ambayo lazima itegemee maslahi ya kitaifa.

“Hii leo, akiwa na mawazo yale yale ya zamani, Rais wa Marekani [Donald Trump] anajaribu kujadiliana na kunyakua uhuru na ustawi wa taifa la Iran kupitia ahadi hewa na michezo ya kisiasa,” ameongeza Mohammad Baqer Qalibaf.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *