MAKAMU wa Pili wa Rais- Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amezitaka taasisi, wadau na wananchi kushirikiana katika kuongeza ubunifu wa upatikanaji wa fedha na vifaa muhimu ili kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.

Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni, Hemed alisema changamoto za kifedha zinazosababisha upungufu wa rasilimali zinachangiwa na kuyumba kwa uchumi wa dunia, kuibuka kwa milipuko ya magonjwa na machafuko katika baadhi ya nchi.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa mpango endelevu wa kudhibiti UKIMWI ili kufikia lengo la kumaliza maambukizi mapya ifikapo 2030. Kwa mujibu wa takwimu, Zanzibar imepiga hatua kubwa katika miongo mitatu iliyopita, na kiwango cha maambukizi kimeshuka hadi asilimia 0.4, sawa na watu takribani 10,256.

Hata hivyo, amesema bado zipo changamoto zinazohitaji juhudi za pamoja, ikiwemo upungufu wa rasilimali na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU. Hemed alisisitiza kuwa maadhimisho ya siku hiyo yanatoa fursa ya kutathmini hatua zilizopatikana na kuhimiza jamii kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi.

Aidha, ametangaza kuwa serikali itaongeza bajeti kwa ajili ya watu wanaoishi na VVU ili kuhakikisha wanapata huduma stahiki ikiwemo dawa za ARV. Aliitaka jamii kuacha unyanyapaa kwani unadhoofisha jitihada za kitaifa.

Taarifa ya Hali ya UKIMWI Zanzibar

Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC), Dkt. Ali Salim Ali, alisema serikali kwa kushirikiana na washirika inaendelea kutoa huduma muhimu ikiwemo elimu ya VVU. SOMA:NIMR yaja na utafiti wenye virusi vya Ukimwi, kisukari

Alisema mwaka huu jumla ya watu 105,056 walipimwa, ambapo 53,559 ni wanawake na 47,397 wanaume. Kati yao, watu 9,607 waligundulika na VVU. Aliongeza kuwa kundi la umri wa miaka 25–49 ndilo linaoongoza kwa maambukizi likichangia asilimia 71.

Kwa upande wa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Dkt. Ali alisema wajawazito 5,331 walipimwa na 89 tu kugundulika na maambukizi. Watoto 362 walipimwa na wawili kugundulika na VVU, hatua aliyosema inaonesha mafanikio makubwa.

Jumuiya ya ZAPHA Yaomba Kuimarishwa kwa Mifumo

Mwakilishi kutoka jumuia ya watu wanaoishi ya Ukimwi Zanzibar (ZAPHA), Sara Abdi Mwita, aliitaka Wizara ya Afya kuunganisha mifumo ya utambuzi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watu wanaoishi na VVU. Alisema mwaka huu kaulimbiu inalenga kuhimiza ongezeko la fedha kwa ajili ya kuendeleza mapambano, na kukabili vikwazo vinavyoongezeka.

Jumuiya hiyo pia ilieleza kukabiliana na changamoto za kusimamishwa kwa baadhi ya shughuli zake, na kuiomba serikali kuimarisha mazingira ya uendeshaji kwa mujibu wa sheria.

UNAIDS Yapongeza Hatua za Zanzibar

Mwakilishi wa UNAIDS, George Anthony, alieleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa hadi kufikia kiwango chini ya asilimia moja cha maambukizi. Hata hivyo, alisema baadhi ya makundi bado yana viwango vya juu vya maambukizi na hivyo mikakati zaidi inahitajika.

Amesema safari ya kumaliza UKIMWI inahitaji kuimarishwa kwa huduma jumuishi, kupaza nguvu za taasisi za kijamii, kuweka usawa wa upatikanaji wa huduma, na kuwekeza katika ubunifu. Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu: “Tuvishinde Vikwazo vya Kifedha, Tuimarishe Mapambano ya UKIMWI.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *