Dar es Salaam. Kati ya wanamuziki waliojaliwa sauti nzuri kutokea katika Bongofleva, basi Maua Sama naye yumo na amedhihirisha hilo kupitia nyimbo zake mahiri ambazo zimesikika kwa miaka zaidi ya 10 sasa.
Anafanya vizuri akiimba miondoko ya RnB na Afropop ambayo kwake ipo kibiashara zaidi, lakini bado mashabiki wanaelewa na kukipa heshima kile anachofanya kwa muda wote. Fahamu zaidi.
1. Tangu ametoka kimuziki kupitia wimbo wake, So Crazy (2013), Maua Sama hajatoa albamu ila amefanikiwa kuachia Extended Playlist (EP) mbili, Cinema (2022) na Sama (2024), ambazo zina upekee wake.
2. Moja ya upekee wa EP zake, ni kwamba zote amemshirikisha staa wa Kings Music, Alikiba, mshindi wa MTV EMAs 2016 kama Msanii Bora Afrika.
Katika EP ya kwanza, Cinema (2022), Alikiba alisikika katika wimbo ‘Nioneshe’ ambao ulifanya vizuri, na katika EP ya pili, Sama (2024), Kiba kashirikishwa katika wimbo ‘Itakuwaje’ ambao pia umebamba.
3. Jina la Maua Sama lilichomoza baada ya kuachia ngoma, So Crazy (2013) akimshirikisha Mwana FA (Hamisi Mwinjuma) ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
4. Kabla kurekodi na Mwana FA, rapa aliyetoka na kibao chake, Ingekuwa Vipi (2002), Maua Sama aliwatumia wimbo huo wasanii kadhaa akiwemo Alikiba, Ommy Dimpoz na Ben Pol ili wote hakuwapata.
5. Mtayarishaji muziki kutokea MJ Records, Marco Chali ambaye pia alitolewa na Mwana FA baada ya kutengeneza (re-recording) ngoma yake, Binamu (2008), ndiye alitengeneza wimbo huo wa Maua Sama.
Ikumbukwe ‘Binamu’, Mwana FA alikuwa ashaurekodi miaka mingi nyuma na ulikuwepo katika albamu ya pili, Toleo Lijalo (2003), ila akaja kuurudia tena kwa Chali kitu kilichompa umaarufu mtayarishaji huyo.
6. Naye Mwana FA alikuja kumshirikisha Maua Sama katika nyimbo zake tatu, Hata Sielewi (2017), Gwiji (2020) na Sio Kwa Ubaya Remix (2022) ambao toleo la awali alisikika Harmonize kutokea Konde Music.
7. Baada ya Maua Sama kuvuma na wimbo huo (So Crazy), alijiunga na Tanzania House of Talent (THT) ili kujifunza muziki na ndipo hapo akaibuka na wimbo wake, Mahaba Niue (2016) uliompaisha zaidi.
8. Wimbo wa Maua Sama, Iokote (2018) ambao video yake ndio imefanya vizuri YouTube kwa upande wake ikitazamwa zaidi mara milioni 32, haukuwa katika mipango yake mikubwa kwa mwaka huo.
9. Wimbo uliokuwa katika mipango yake ni Amen (2018) akishirikiana na Ben Pol, ila Iokote (2018) ulipotoka muda mfupi baadaye ukafanya vizuri na kumpatia show nyingi kiasi cha kununua gari lingine.
Hata hivyo, Maua Sama alishauriwa asimuweke Hanstone katika wimbo huo (Iokote) kutokana hakuwa msanii mkubwa ila Maua akasema ngoja ampe nafasi kama Mwana FA alivyomkubalia kolabo akiwa hajulikani.
10. Hanstone, mtoto wa mwanamuziki marehemu Banza Stone, baada ya kolabo hiyo na Maua Sama akawa maarufu katika Bongofleva hadi ‘kusainiwa’ na lebo ya WCB Wasafi ingawa mambo yalikuja kuvurugika kabla hata ya kutambulishwa!.