Uingereza. Mwimbaji mkongwe wa muziki duniani kutoka Uingereza, Sir Elton John amefichua amekuwa akipambana na hali ya upofu kwa takriban miezi 15 iliyopita.

John, 78 alipata maambukizi ya jicho Julai mwaka jana, yaliyomfanya kutoona kabisa kwa jicho lake la kulia.

Pia alifichua, hata jicho lake la kushoto lina uwezo mdogo sana wa kuona.

Mapema mwaka huu, alipoongelea hali yake amesema hajaruhusu changamoto hiyo kumvunja moyo.

“Nina matatizo makubwa ya macho kwa sasa. Kuna siku nimejisikia vibaya, lakini kisha najikumbusha jinsi nilivyo mwenye bahati,” amesema Elton aliyeanza kujishughulisha na muziki tangu mwaka 1962.

Hata hivyo, amesema anaendelea kuwa na matumaini uoni wake utaboreshwa katika miezi ijayo.

“Sasa nina heshima mpya kwa watu wenye uoni hafifu na wale ambao hawaoni kabisa, baadhi yao ninawasiliana nao. Lakini basi, nina maisha mazuri na nina matumaini kuona kwangu kutaimarika,” amesema mkongwe huyo.

Katika mahojiano na Gazeti la The Guardian, mwimbaji huyo wa Rocket Man amesema tayari amewahi kushinda uraibu na changamoto nyingine za kiafya, hivyo hata hali hii haitamshinda.

“Hali hii hainishindi. Nimeshinda uraibu, nimeshinda matatizo ya afya na ninaweza kujinyanyua na kuendelea mbele,” amesema.

Hivi karibuni, John alitangazwa Philanthropist wa Mwaka 2025 na jarida Variety na kupitia mitandao yake ya kijamii, alizungumza pia kuhusu jinsi alivyopoteza watu wengi aliowapenda, akiwemo rafiki yake Ryan White kutokana na UKIMWI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *