Kisukari kinahitaji kila rika kujilindaKisukari kinahitaji kila rika kujilinda

KISUKARI ni ugonjwa unaotokea pale mwili unaposhindwa kuzalisha homoni ya insulini kwa kiasi cha kutosha au unaposhindwa kutumia vizuri homoni hiyo iliyozalishwa mwilini.

Kwa mujibu wa wataalamu, homoni hiyo ndiyo inayohusika kushughulika na kiwango cha sukari kwenye damu na namna kinavyotumika.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinabainishwa kuwa kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa sukari kwa zaidi ya miongo mitatu.

Taarifa ya WHO kuhusu ugonjwa wa Kisukari inafafanua kuwa mwaka 2022 asilimia 14 ya watu wa umri wa miaka 18 na kuendelea walikuwa wakiishi na Kisukari, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7 kutoka mwaka 1990.

Inaelezwa kuwa asilimia 59 ya watu hao hawakuwa wakifata matibabu katika kipindi hicho na kwamba matibabu yalikuwa ni ya kiwango cha chini katika nchi zenye kipato cha kati.

Kufikia mwaka 2021 Kisukari ndiyo kilikuwa chanzo cha moja kwa moja cha vifo milioni 1.6 na asilimia 47 ya vifo vinavyotokana na kisukari vilivyotokea kabla ya umri wa miaka 70.

Taarifa hiyo inasisitiza kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na kisukari imekuewa ikiongezeka tangu mwaka 2000.

Novemba 14, kila mwaka dunia inaadhimisha Siku ya Kisukari Duniani ambayo hutoa fursa ya kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo sambamba na kueneza maarifa na ufahamu ili kusaidia kuleta mabadiliko ya kudumu kwa wote walioathirika na ugonjwa huo.

Wakati wa maadhimisho ya mwaka huu, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani (ikiwemo Kisukari) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Mloganzila, Sania Kasiandu anaeleza kuhusu ugonjwa huo na kusema kuwa ni ugonjwa usioambukiza unaompata mtu kama matokeo ya homoni ya insulini kushindwa kuzalishwa au kutumika ipasavyo mwilini.

“…kiwango cha sukari kwenye damu kinakuwa juu kuliko kawaida, kwa sababu mwili hauzalishi insulini ya kutosha au hautumii insulini ipasavyo.”

Dk Kasiandu anaeleza kuwa kuna aina mbalimbali za kisukari lakini ziko mbili ambazo ndiyo zinazofahamika zaidi.

Type 1 (aina ya kwanza) ni ile ambayo mwili umeshindwa kabisa kutengeneza insulini na hii huanza utotoni au kwa kijana, mgonjwa anategemea tiba ya insulini maisha yake yote. Aina ya pili, mwili unatengeneza insulini lakini haiitumii vizuri, kitu ambacho kinajulikana kitaalamu kama insuline resistance (upinzani wa insulini). Hapo zamani ilikuwa inaonekana kwa wazee lakini sasa vijana wengi wanaipata.”

Dalili za sukari

Dk Kasiandu anasema haijalishi mgonjwa anaugua aina gani ya kisukari, dalili zote zinafanana.

“Dalili kuu zinazoweza kuwapata watu wengi zinaweza kuwa ni kukojoa mara kwa mara, kusikia kiu kali au njaa kali, kupungua uzito na kuchoka mara kwa mara,” anasema

Akieleza sababu za mtu kuugua kisukari, Dk Kasiandu anasema sababu zinatofautiana, kulingana na aina ya kisukari na kufafanua kuwa aina ya kwanza inatokea pale mwili unapohisi kongosho ni adui na kinga ya mwili inaanza kupingana na kongosho, kwa hiyo kongosho linakuwa halina uwezo tena wa kutengeneza insulini na hapo mtu anaweza kupata kisukari cha aina ya kwanza.

Anaongeza kuwa, sababu nyingine inaweza kuwa vinasaba vya mtu.

Aidha, kwa upande wa aina ya pili ya kisukari anasema, “…jinsi tunavyoishi maisha yetu, kula vibaya, kutofanya mazoezi, kunywa pombe sana na kadhalika.”

Anasema watu wanaweza kuepuka kisukari kwa kupunguza uzito kupita kiasi.

“Ukipunguza uzito kwa asilimia tano mpaka saba, hupunguza hatari ya kupata kisukari kwa kiwango kikubwa. Kitu cha pili ni kula chakula chenye lishe bora, punguza vyakula vya kukaanga, vyenye sukari nyingi kama juisi, soda, chokleti au keki na uongeze mboga, matunda na nafaka zisizo kobolewa.”

Anaongeza kuwa, mtu anapaswa kula protini za kama samaki, kuku, maharage na kula nyama nyekundu kama nyama ya ngombe na nguruwe kwa kiwango kidogo sambamba na kupunguza kula wanga, hasa uliosindikwa ili kujiweka katika hali ya usalama wa kupata kisukari.

“Kitu kingine ni kufanya mazoezi mara kwa mara. Mazoezi yanasaidia mwili kutumia insulini vizuri. Angalau dakika 30 za kutembea kwa kasi mara tano kwa wiki au kuogelea, kupanda ngazi, kuendesha baiskeli, hata kutembea dakika 10 baada ya mlo kunasaidia sana kupunguza sukari. Hapa namaanisha, dakika 10 baada ya kifungua kinywa, dakika 10 baada ya mlo wa mchana na dakika 10 baada ya mlo wa usiku, jumla hapo ni dakika 30 kwa siku,” anasema.

Anataja mambo mengine kuwa ni kudhibiti msongamano wa mawazo, kupunguza au kuacha kunywa pombe kupita kiasi, kupunguza matumizi ya vinywaji vyenye sukari, kama soda na juisi, kulala muda wa kutosha usiopungua saa saba mpaka tisa kwa siku.

“Usingizi mdogo husababisha kuongeza uzito na insuline resistance.”

Aidha, anasema kisukari kinaweza kuathiri watu katika hatua zote za maisha, ikiwa ni pamoja na utoto, miaka ya uzazi, umri wa kufanya kazi na utu uzima.

Naye Daktari, Dimon Bernad anasema ukiachana na sababu nyingine zinazosababisha mtu kupata kisukari, mitindo ya maisha inachukua nafasi kubwa katika ongezeko la wagonjwa kisukari, jambo ambalo ni hatari kwa kuwa kisukari kinaambatana na changamoto nyingine za kiafya.

Anasema asilimia kubwa ya magonjwa ya figo (ingawa hataji takwimu) yanatokana na tatizo la kisukari, hivyo jamii inapaswa kuwa makini katika kukabiliana na ongezeko la kisukari.

Anaongeza kuwa, kisukari kinaambatana pia na ukosefu wa nguvu za kiume, uoni hafifu na mwili kukosa nguvu ya kufanya kazi kwa ufasaha.

Dk Bernad anashauri jamii kuona umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa kuacha kula vyakula hatarishi kama mafuta na sukari kupitiliza sambamba na kuweka ratiba za kufanya mazoezi katika shughuli zao za kila siku.

Ujumbe wa WHO katika maadhimisho ya mwaka huu unasema Kaulimbiu ya mwaka huu, “Kisukari Katika Hatua Mbalimbali za Maisha” inatambua kuwa kila mtu anayeishi na ugonjwa wa kisukari anapaswa kupata huduma jumuishi, mazingira ya usaidizi na sera zinazokuza afya, utu na kujisimamia.

Kampeni hii inasisitiza umuhimu wa mbinu ya maisha kwa kuzuia, kudhibiti na ustawi wa jumla kwa wenye kisukari.

Aidha, ujumbe huo unasisitiza kuwa ugonjwa huo unaweza kumpata mtu yeyote kuanzia utotoni, ujana hadi uzee, hivyo kusaidia ustawi na kujitunza kutasaidia watu wenye ugonjwa wa kisukari katika kila umri.

Mwisho

@@@@@@

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *