Dar es Salaam. Hatima ya uhalali wa kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sasa itajulikana Februari 2026, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam itakapoamua pingamizi dhidi ya kesi hiyo.

Tarehe ya uamuzi huo imepangwa leo Jumatatu, Desemba 1, 2025, na Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo, wakati ilipotajwa.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Wadaiwa ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Wadai wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kesi hiyo ilipotajwa Septemba 29, 2025, wadaiwa waliibua pingamizi la awali wakihoji mamlaka ya mahakama hiyo kuisikiliza.

Wanaiomba mahakama hiyo iitupilie mbali bila kuisikiliza, wakidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza, huku wakibainisha sababu saba za pingamizi hilo.

Pamoja na mambo mengine, katika pingamizi hilo wadaiwa wanadai madai ya wadai yanahusu mambo ya kikatiba, lakini kesi hiyo imefunguliwa kama kesi ya madai ya kawaida badala ya kesi ya kikatiba.

Mahakama hiyo ilielekeza pingamizi hilo lisikilizwe kwa njia ya maandishi, na ikapangwa itajwe leo ili kuangalia kama pande zote zimeshawasilisha hoja zake na kupanga tarehe ya uamuzi.

Leo ilipoitwa, kiongozi wa jopo la mawakili wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala, ameieleza mahakama kuwa wao tayari walishawasilisha hoja zao, lakini upande wa wadai hawajapewa majibu ya wadai, hawa wanadai wameshayawasilisha kwenye mfumo wa mahakama wa usimamizi wa mashauri.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, Shaban Marijan ambaye anasaidiana na mawakili Gido Simfukwe na Alvan Fidelis, amekiri bado walikuwa hawajawapatia upande wa wadaiwa nakala ya hati ya majibu yao.

Hata hivyo, ameihakikishia mahakama kuwa kweli walishawasilisha majibu yao kwenye mfumo wa mahakama, huku akiomba waongezewe muda mfupi tu kuwapatia wadaiwa majibu yao leo hii.

Jaji Mwanga, baada ya kujiridhisha kuwa tayari majibu ya wadai yako kwenye mfumo wa mahakama, amekubaliana na ombi la wakili Marijan na ameelekeza wadai wawapatie nakala ya majibu yao wadaiwa.

Hivyo, ametoa siku mbili kwa wadaiwa kuwasilisha mahakamani majibu ya nyongeza dhidi ya majibu ya wadai kama wanaona umuhimu wa kufanya hivyo.

Pia Jaji Mwanga amepanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Februari 17, 2026 au kabla ya tarehe hiyo kama atapata nafasi, ambayo pande zote watajulishwa, kufuatia maombi ya upande wa wadaiwa kuwa wapangiwe muda wa karibu.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, naye amewasilisha maombi akiomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo kama mdaawa mwenye maslahi.

Maombi hayo pia yametajwa mahakamani hapo leo bila Lissu mwenyewe kuwepo.

Hata hivyo, mahakama imewapa siku sita wajibu maombi ambao ni Said na wenzake (wadai katika kesi ya msingi) kwa upande mmoja, na Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu ambao ni wadaiwa katika kesi ya msingi, kuwasilisha viapo kinzani kujibu maombi hayo ya Lissu.

Jaji Mwanga ameelekeza wawasilishe mahakamani hapo viapo hivyo kabla au kufikia Desemba 8, 2025, huku akipanga kusikiliza maombi hayo Februari 17, 2026, kutegemeana na uamuzi wa pingamizi la Chadema dhidi ya kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanaomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019, na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.

Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika, pamoja na gharama za kesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *