Manchester United imeanza kumuangalia kiungo wa kati wa Bournemouth, Tyler Adams, katika dirisha la usajili la Januari au msimu ujao wa joto, huku dau lake likikadiriwa kufikia pauni milioni 40.

Adams mwenye umri wa miaka 26 raia wa Marekani, alikuwa na mchezo mzuri jana usiku wakati Bournemouth ilipokuwa ugenini dhidi ya Man United katika mechi iliyomalizika kwa sare ya mabao 4-4 kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Jina la Adams limekuwa likitajwa kwenye mijadala ya ndani ya United kuhusu kuimarisha safu ya kiungo, ambapo anaonekana kuwa chaguo nafuu ikilinganishwa na majina mengine yanayotajwa kama Carlos Baleba, Elliot Anderson na Adam Wharton.

Akizungumza jana kabla ya mchezo huo, Adams alisema kucheza Old Trafford ni ndoto kubwa ya kucheza Ligi Kuu England.

“Ni tukio la kipekee. Huu ni uwanja niliokua nikiutazama tangu utotoni. Hata kama wewe si shabiki wa United, kuingia Old Trafford kunabadilisha kabisa mtazamo wako.

“Niliwahi kucheza hapa wakati wa Covid nikiwa na RB Leipzig. Nilipoingia Old Trafford mara ya kwanza nikajikuta nikisema, ndoto yangu ni kucheza Ligi Kuu ya England kwa sababu hapa ndipo soka halisi lilipo.

Sasa kurudi kucheza hapa mara kadhaa na kupata matokeo mazuri kunafanya niwe bora zaidi,” alisema Adams.

Adams ni kiungo namba sita mwenye uwezo mkubwa akiwa ndiye kiungo aliyedhibiti mashambulizi ya wapinzani mara nyingi zaidi katika msimu huu wa EPL akizidiwa na Moises Caicedo wa Chelsea.

Mbali na majukumu yake ya ukabaji, Adams alionyesha uwezo wa kushambulia mwezi uliopita alipofunga bao la kuvutia dhidi ya Sunderland, akimpiga chenga kipa Robin Roefs na kuachia shuti la mita karibu 50 kutoka katikati ya uwanja.

Bao hilo lilichaguliwa kuwa bao bora la mwezi Novemba.

“Ulikuwa ni wakati wa kujikuta tu, nikasema nijaribu,” alisema Adams baada ya kufunga bao hilo.

“Kama utanipa nafasi hiyo mara 10 hata bila kipa, labda mara mbili tu nitapiga kwa usahihi ule. Lakini ni muhimu kuongeza kitu kipya kwenye mchezo wako bila kusahau majukumu yako ya msingi ya ulinzi.”

Licha ya kiwango kizuri cha Bournemouth chini ya kocha Andoni Iraola, timu hiyo licha ya kupata sare kwenye mchezo dhidi ya United bado haijashinda katika mechi saba mfululizo, ikipoteza nne.

Hata hivyo, Adams amesema hana hofu, akisisitiza kuwa morali ya kikosi ni muhimu zaidi.

“Nimewahi kuwa kwenye timu iliyoshuka daraja. Naweza kusema morali ya timu ina maana kubwa sana. Lazima ubaki chanya, ufanye kazi kwa bidii na mambo yatabadilika,” amesema Adams.

Kiungo huyo ambaye ni nguzo ya timu ya taifa ya Marekani, anatazamia majira ya kiangazi yenye shughuli nyingi wakati Kombe la Dunia litakapofanyika Amerika Kaskazini. Huenda ikawa majira ya kipekee zaidi iwapo Manchester United itaamua kuwasilisha ofa rasmi mezani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *