Dar es Salaam.  Katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili, jamii  imelazimika kuunda umoja ili kusaidia kukumbusha asili, mila na desturi ili kujenga maadili kwa vijana.

Umoja huo wa wanaukoo wa Bichwabuta kutoka Bukoba mkoani Kagera, pamoja na mambo mengine unalenga kukumbusha asili ya jamii hiyo, wakiamini ni njia rafiki ya kuwarejesha vijana kwenye maadili na kuwakumbusha asili yao.

Mwenyekiti wa umoja huo,  Creus Kyoma amesema kama jamii wanahitaji kukaa na vijana ili kuwakumbusha chimbuko na asili yao sanjari na  kujua mila na desturi zao ukoo huo wa kabila la Wahaya.

“Tunafahamu kuna  mmomonyoko mkubwa wa maadili, hivyo kama wanaukoo tumeitana ili tufahamiane na kudumisha mila zetu na kuweka mikakati ya kukumbusha asili yetu,” amesema. 

Awali katibu wa umoja huo, Godfrey Kazinja alisema wameungana kuwajenga vijana wa jamii hiyo na wengine katika kutambua asili na chimbuko lao.

“Tumeona kuna  mmomonyoko wa maadili, vijana wengi wanaenenda  vibaya na wengi wao  wanafanya maamuzi hatari na kuingia kwenye majanga.

“Hivyo umoja huu tumejikita kuwajenga ili kufikia hatma njema ya vizazi vyetu vijavyo,” amesema.

Amesema katika umoja huo watahakikisha vizazi vya asili yao havipotei wakilinda mila na  utamaduni wa jamii hiyo.

Mbali na maadili, amesema pia wamejikita kwenye uchumi kwa kuanzisha mfuko wa kuchangishana kutatua changamoto kadha wa kadha za wana umoja.

Naye mweka hazina wa umoja huo, Rosemary Kazinja amesema vijana wao wengi hawafahamu vitu vingi vya mila na desturi kwa kuwa wamezaliwa mijini.

“Kwa umoja huu itasaidia kuwajenga vijana waweze kujua chimbuko lao, lakini pia kusaidiana katika masuala mbalimbali ya kijamii,” amesema.

Akifafanua namna ya kujiunga na umoja huo, mhamasishaji wake, Omary Lurengwa amesema ukoo wa Bichwabuta ni mkubwa na umetawanyika sehemu nyingi duniani na wengi wao hawafahamiani.

“Popote walipo wanaweza kujikusanya kama ambavyo sisi tumefanya Dar es Salaam  na baada ya muda tutakutana ki nchi tukiwa wengi zaidi na kuendeleza lengo la kuwaunganisha vijana,  kuwapa morali, kuwakumbusha utamaduni na nidhamu ya jamii yetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *