Siku ya Jumanne (Disemba 16), Urusi iliukataa wito wa Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani aliyemtaka Rais Vladimir Putin kusitisha mapigano katika msimu wa Krismasi, wakati huu juhudi za kidiplomasia zikiendelea kuvikomesha kabisa vita hivyo. 

Akinukuliwa na mashirika ya habari ya Urusi muda mfupi baada ya wito huo wa Kansela Merz, msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, alisema nchi yake inataka amani ya kweli na ya kudumu, na sio usitishaji pekee wa mapigano.

“Ikiwa Ukraine inasaka masuluhisho ya kitambo na yasiyo endelevu, hapana shaka sisi hatuko tayari kushiriki kwenye hayo. Tunataka amani – hatutaki makubaliano yatakayoipa Ukraine ahuweni na muda wa kujiandaa kuendeleza vita. Tunataka kukomesha vita hivi, kufikia malengo yetu, kulinda maslahi yetu, na kuhakikisha amani ya Ulaya kwa siku zijazo.” Alisema Peskov.

Kauli hiyo ya Kremlin  ilitanguliwa na maamuzi ya mkutano wa pande tatu mjini Berlin, Ujerumani, ambapo wanadiplomasia wa Ukraine, Ulaya na Marekani walikusanyika kwa siku mbili kwa ajili ya mazungumzo ya amani ya Ukraine yaliyodhamiriwa kuvimaliza vita vilivyotokana na uvamizi wa Urusi wa Februari 2022. 

Kwenye tamko lao la pamoja la jioni ya Jumatatu (Disemba 15), viongozi wa Ulaya walitowa wito wa kuundwa kwa kikosi cha kimataifa ili kuhakikisha usitishaji mapigano nchini Ukraine.

Ujerumani Berlin 2025 | Mkutano wa Ukraine
Viongozi wa Ulaya, Ukraine na wawakilishi wa Marekani kwenye mazungumzo ya Berlin kukomesha vita vya Urusi dhidi ya Kiev.Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Kwa kuwa wawakilishi wa Urusi hawakualikwa kwenye mazungumzo hayo ya Berlin, Peskov alisema haikuwa imeliona tamko hilo na hivyo asingeliweza kujibu chochote kulihusu.

Tamko hilo, pamoja na mengine, linaipa Ukraine hakikisho la kiusalama kutoka kwa Marekani.

Urusi kukabidhiwa mapendekezo na Marekani

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema kuwa mapendekezo hayo yanayosimamiwa na maafisa wa Marekani kwa ajili ya kupatikana mkataba wa kukomesha vita vya miaka minne vya Urusi, yangeliweza kukamilishwa ndani ya siku chache zijazo na kisha wajumbe wa Washington kuyafikisha Kremlin kabla ya mkutano mwengine unaowezekana kufanyika mwishoni mwa wiki ijayo nchini Marekani.

Zelensky aliwaambia waandishi wa habari kwamba hata kama “rasimu ya mpango huo wa amani iliyojadiliwa mjini Berlin siku ya Jumatatu si kamilifu lakini inatekelezeka.”

Ujerumani Berlin 2025 | Volodymyr Zelensky na Friedrich Merz
Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani (kulia) na mgeni wake, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine wakiwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo ya Berlin.Picha: Halil Sagirkaya/Anadolu Agency/IMAGO

Hata hivyo, alisema baadhi ya masuala muhimu – kama vile kitakachojiri kwa eneo la Ukraine linalokaliwa kimabavu na vikosi vya Urusi – yalikuwa bado hayajapatiwa ufumbuzi.

Kwenye mkutano huo wa Berlin, Marekani iliipa Ukraine ahadi ya hakikisho la usalama kama lile walilonalo wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, licha ya kwamba Ukraine si mwanachama wa Muungano huo. 

Hata hivyo, ahadi hiyo inakwendana na sharti la Ukraine kukubali kuyaachia madai yake kwa maeneo ambayo tayari yametwaliwa na Urusi, hasa mikoa ya Donetsk na Luhansk, suala tete kabisa kwa siasa za ndani na kikanda kwa Ukraine na Ulaya nzima.

Ulaya yaanzisha kamisheni ya kimataifa kufidia madhara ya vita

Hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya umeanzisha Kamisheni ya Kimataifa ya Madai ya Ukraine katika juhudi za kuhakikisha kuwa Kiev inafidiwa kwa mabilioni ya dola kutokana na madhara iliyoyapata kwa mashambulizi ya Urusi na uhalifu wa kivita dhidi yake. 

2025 | Kaja Kallas
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, anasema lazima suala la fidia liendane sambamba na hatua za usalama kwa Ukraine na Ulaya.Picha: Virginia Mayo/AP Photo/dpa/picture alliance

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema uanzishwaji wa Kamisheni hiyo unalenga kuhakikisha kuwa Ukraine haitaachwa katika hali iliyo, hata kama makubaliano ya kukomesha yanayotafutwa sasa yatapatikana.

“Pamoja na kupatikana haki kutokana na uvunjwaji mkubwa wa sheria za kimataifa, fidia ni muhimu sana kwa ajili ya uwajibikaji. Na ikiwa kweli tunaamini kwenye amani ya haki na ya uhakika nchini Ukraine na usalama barani Ulaya, lazima tuendelee kupigania uwajibikaji.” Alisema Kallas.

Viongozi 34 wa Umoja huo walikutana mjini The Hague, Uholanzi, hapo jana kutia saini uzinduzi wa Kamisheni hiyo uliohudhuriwa pia na Rais Zelensky. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *