Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS ameushutumu utawala wa kizayuni wa Israel kwa ukiukaji mkubwa na uliopangwa wa makubaliano ya kusitisha vita, akionya kwamba kuendelea kwa mwelekeo huu kunayaweka makubaliano hayo katika hatari ya kuvunjika kikamilifu.

Ghazi Hamad, ametangaza kuwa, utawala wa Kizayuni “umeyachezea” maandiko ya makubaliano ya kusitisha mapigano na haujakiacha kifungu chochote cha makubaliano hayo kikiwa hakijavunjwa au kubadilishwa.

Akiashiria tathmini iliyotolewa na wapatanishi, Hamad ameeleza kwamba, wapatanishi wametamka bayana kuwa Hamas haijakiuka makubaliano hata mara moja na imetekelezwa kikamilifu vipengele vyake.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas, kurudiwa kila mara ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha vita unaofanywa na utawala wa kizayuni kunaonyesha kwamba vitendo hivyo “vinapangwa na kutekelezwa kwa uamuzi wa baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu”.

Amesema, ukiukaji huo ni pamoja na mauaji, kuwanyonga watu ugani, kuwafyatulia risasi raia, mashambulizi ya makombora na kuwaua watu kwa kuwalenga, na kwamba vikosi vya utawala ghasibu wa kizayuni vimekiuka mara kadhaa mipaka iliyoainishwa; ambapo katika baadhi ya matukio, ukiukaji huo umesonga mbele ndani ya Ghaza kwa takribani kilomita mbili.

Ghazi Hamad amebainisha pia kwamba tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipoanza kutekelezwa, zaidi ya matukio 813 ya ukiukaji uliofanywa na jeshi la kizayuni yamerekodiwa, ukiwa ni wastani wa matukio 25 kwa siku.

Kiongozi huyo wa Hamas ametahadharisha kwamba ukiukaji huo wa “waziwazi” unatishia makubaliano hayo kwa uzito mkubwa na kuyaweka katika hatari ya kuvunjika kikamilifu, na kwamba wapatanishi wanapaswa wachukue hatua madhubuti ili kuuzuia utawala wa kizayuni usiendelee na mwenendo huo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *