
Mkuu wa wafanyakazi wa Ikulu ya Marekani White House Susie Wiles ametamka kuwa, mashambulizi ya jeshi la Marekani dhidi ya boti zinazodaiwa kuwa ni za madawa ya kulevya yanayofanywa katika eneo la Amerika Kusini yanalenga hatimaye kumpindua Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.
Matamshi hayo ya Wiles yaliyochapishwa na jarida la Vanity Fair siku ya Jumanne, yameonekana kupingana waziwazi na hoja ambayo imekuwa ikitolewa na serikali ya rais wa Marekani Donald Trump kama sababu hasa ya kuanzisha mashambulizi hayo ya kijeshi, yaani kupambana na mihadarati.
“Yeye [Trump] anataka aendelee kuziripua boti mpaka Maduro ajisalimishe. Na watu werevu zaidi kuliko mimi kuhusiana na hilo, wanasema atafanya hivyo,” Wiles amenukuliwa akisema.
Jarida la Vanity Fair lilitoa maelezo marefu kuhusu Wiles jana Jumanne, saa chache baada ya Pentagon kutangaza kufanyika mashambulizi mengine matatu dhidi ya boti katika Bahari ya Pasifiki Mashariki ambayo ilisema yaliua watu wanane.
Kufuatia ungamo hilo la waziwazi la msaidizi mwandamizi wa Trump, Seneta wa chama cha Democratic Chris Murphy ameandika kwenye mtandao wa X: “kwa hivyo si vita dhidi ya magenge. Ni kubadilisha utawala,” na akaongezea kwa kusema: “vyovyote itakavyokuwa, ni kinyume kabisa cha sheria na ni (hatua) ya kipuuzi”.
Serikali ya Washington imekuwa ikishadidisha mashambulizi dhidi ya vyombo vya majini sambamba na kuzidi kujizatiti kijeshi karibu na Venezuela, na kuibua shaka kwamba lengo la hatua hizo linaweza likawa ni kupanga vita vingine vya kubadilisha utawala kwa nguvu za kijeshi dhidi ya serikali ya mrengo wa kushoto ya Maduro.
Katika kipindi cha miezi kadhaa ya karibuni, Trump amesisitiza mara kadhaa kwamba “siku za rais wa Venezuela zinakaribia ukingoni”.
Hii ni katika hali ambayo, kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne jioni, Makamu wa Rais wa Venezuela Delcy Rodríguez amesema nia hasa ya Marekani ni “kutwaa mafuta, ardhi, na madini ya Venezuela.”
Hata hivyo, Bi Rodríguez amesisitiza kwa kusema: “Venezuela haitakuwa tena katu koloni la dola kuu au dola lolote la kigeni”…/