
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi amesisitizia azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya kutetea haki zake za kisheria za nyuklia kulingana na Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), akisema sera za nyuklia za Tehran zingali zinaendana na mfumo wa sheria za kimataifa.
Araghchi, ambaye anaitembelea Moscow baada ya safari yake ya Belaruss, ameyasema hayo katika mkutano na wanasiasa, wataalamu, na wasomi wenye vipawa wa Russia jana Jumanne, ambapo alizungumzia uhusiano kati ya Iran na Russia na matukio muhimu ya kimataifa.
Katika hotuba yake hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha msimamo wa Tehran kuhusu masuala ya kimataifa, hususan yanayohusiana na amani na usalama wa kimataifa.
Akizungumzia kadhia ya nyuklia ya Iran, Araghchi amehusisha hali ya sasa na ukiukaji wa mara kwa mara wa ahadi na wajibu ambao umefanywa na Marekani na kujihusisha nchi tatu za Ulaya katika utekelezaji wa “hatua haramu” za Washington, hasahasa hatua yake ya upande mmoja ya kujiondoa mwaka 2018 katika makubaliano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ya 2015 na uvamizi wa kijeshi uliofuatia hatua hiyo ambao ulifanywa dhidi ya Iran mnamo mwezi Juni 2025.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametilia mkazo pia umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Tehran na Moscow, na kubainisha nafasi ya suala hilo katika kuendeleza maslahi ya taifa ya nchi zote mbili na kudumisha amani na usalama wa kimataifa.
Aidha, amesisitizia azma ya pamoja iliyoonyeshwa na viongozi wa mataifa hayo mawili ya kupanua ushirikiano katika nyanja zote.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Araghchi leo amepangiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov, ambapo wawili hao wanatazamiwa kujadili masuala ya kimataifa yanayojiri hivi sasa, ikiwa ni pamoja na mpango wa nyuklia wa Iran na masuala ya kikanda yenye maslahi kwa pande mbili…/