
KOCHA wa zamani wa Azam FC aliyekuwa akiinoa Wiliete Banguela ya Angola kabla ya kuondolewa hivi karibuni, Mfaransa Bruno Ferry yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na Rayon Sports ya Rwanda, ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu alipoachana na Wiliete, Novemba 15, 2025.
Kocha huyo aliachana na Wiliete, baada ya ripoti kutoka Angola kudai mabosi wa kikosi hicho walishindwa kumpatia kibali kazi (work permit), kinyume cha sheria hivyo, kusitishiwa haraka mkataba na kurejea kwao Ufaransa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ferry alisema ataweka wazi makubaliano yatakapofikiwa, ila kwa sasa asingependa kuelezea ni timu gani atakayojiunga nayo, licha ya kukiri ni kweli mazungumzo na miongoni mwao yapo na yanaendelea vizuri hadi sasa.
“Sio uungwana mimi kusema klabu nitayoenda kwa sababu sio rasmi, nafikiri tusubiri hadi pale itakapokamilika, ingawa ni kweli kuna mazungumzo hayo yanaendelea japo kuhusu ni timu ya nchi gani hilo tuliache kwanza kwa sasa,” alisema Ferry.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kocha huyo anatarajiwa kuwasili muda wowote Rwanda kwa ajili ya kuanza majukumu na kikosi hicho, ambapo inaelezwa atashirikiana kwa ukaribu na makocha wawili wasaidizi, ambao ni Lomami Marcel na Haruna Ferouz.
Kibarua cha kwanza kwa kocha huyo, kitakuwa Ijumaa hii ya Desemba 19, dhidi ya Gorilla inayoshika nafasi ya 10 na pointi 15, baada ya kucheza mechi 12, ikishinda tatu, sare sita na kupoteza tatu, ikifunga mabao manane na kuruhusu saba.
Katika Ligi Kuu ya Rwanda, Rayon inashika nafasi ya tano na pointi 17, baada ya kucheza mechi 11, ikishinda tano, sare mbili na kupoteza nne, ikifunga mabao 13 na kuruhusu 12, nyuma ya vinara, Police FC inayoongoza kwa kukusanya pointi 26.
Katika Ligi Kuu ya Angola Girabola msimu huu, Ferry aliiacha Wiliete ikishika nafasi ya pili na pointi zake 13, baada ya kushinda mechi nne tu, sare moja na kupoteza miwili, nyuma ya Petro Atletico inayoongoza hadi sasa ikikusanya pointi 16.
Kocha huyo aliiongoza timu hiyo msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo alitolewa hatua ya kwanza na Yanga kwa jumla ya mabao 5-0, akichapwa nyumbani Angola 3-0, Septemba 19, 2025, kisha 2-0, jijini Dar es Salaam Septemba 27, 2025.
Ferry alijiunga na Azam Julai 5, 2023, akiwa ni kocha msaidizi akishirikiana na Msenegal Youssouph Dabo, ingawa makocha hao waliondoka Agosti 31, 2024, baada ya kuiongoza katika mechi 31 za Ligi Kuu, wakishinda 21, sare saba na kupoteza mitatu tu.