MAAFANDE wa JKT Tanzania wameingilia kati dili la kumpata kwa mkopo nyota wa Yanga, Denis Nkane, baada ya mchezaji huyo anayecheza nafasi mbalimbali uwanjani kushindwa kupenya katika kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa uliopo.

Awali, mabosi wa TRA United walikuwa wa kwanza kumuhitaji nyota huyo baada ya aliyekuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Emmanuel Mwanengo kudaiwa tayari ameshasaini Yanga hivyo, muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa Jangwani.

Hata hivyo, baada ya kiongozi mmoja kudai wanamuhitaji Nkane ila uhamisho huo utategemea na pendekezo la kocha, Mrundi Etienne Ndayiragije, ghafla mabosi wa JKT wameingilia kati na sasa nyota huyo anawaniwa na timu hizo mbili zinazomtaka.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza JKT inamuhitaji mchezaji huyo na muda wowote itawasilisha barua rasmi kwa uongozi wa Yanga, licha ya kutambua wazi inaenda kukutana na ushindani kutokana na klabu mbalimbali pia zinamuhitaji.

“Ni pendekezo moja kwa moja la benchi letu la ufundi ambalo linamuhitaji, tunachokifanya sisi ni kuwasilisha barua yetu ya kumuhitaji kwa mkopo dirisha dogo bila ya kujali ushindani na klabu nyingine zinazomuhitaji,” alisema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo aliliambia Mwanaspoti licha ya kutowasilisha barua hiyo kwa waajiri wake, ila ameambiwa uamuzi wa mwisho wa timu atakayoichezea utabakia pia kwa Nkane mwenyewe, hivyo klabu yenye ushawishi na atakayoihitaji ndiyo atakayoenda.

Nkane anayeweza kucheza beki wa kulia, winga na kiungo mshambuliaji, alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la Januari Mosi 2022, akitokea Biashara United ‘Wanajeshi wa Mpakani’, ambapo kwa sasa hana nafasi kikosini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *