KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu ya Geita (GGML) inatarajia kuanza kulipa fidia kwa wakazi wa mtaa wa Nyakabale mjini Geita ili kupisha leseni ya uchimbaji wa madini ifikapo Januari 2026.

Fidia hiyo ni madai ya zaidi ya miaka 25 ya wakazi wa mtaa huo na maeneo ya jirani ambayo yapo ndani ama yaliyoathirika na leseni kubwa ya uchimbaji ya mgodi wa GGML.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amewasilisha taarifa hiyo katika kikao cha 21 cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika ofisi kwake mjini Geita.

Shigela amesema hatua hiyo imefikiwa kufuatia maridhiano kati ya mgodi wa GGML na serikali ya awamu ya sita chini ya Dk Samia Suluhu ambayo iliahidi kumaliza kilio hicho cha muda mrefu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati.

Amesema mpaka sasa (Desemba 2025) zoezi la uthaminishaji limeshakamilika kwa eneo kubwa na kung’amua kiwango anachostahili kulipwa fidia kila mhusika kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Shigela ameukihakikishia umma kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2026, kila muathirika wa eneo hilo atakuwa ameanza kuwekewa fedha ya fidia kwenye akaunti yake.

Amesema kabla ya GGML kuanza kulipa fidia ofisi ya mkuu wa mkoa inaendelea na taratibu kufanikisha upatikanaji wa eneo mbadala kwa watu wote watakaopisha leseni ya GGML

Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) Geita.

“Tumepanga kupeleka mapendekezo tupate aridhi, tupime viwanja tuwape wananchi wakajenge, na tutapeleka huduma zote ikiwemo maji, umeme, barabara, shule na afya,” amesema.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema tathimini ya GGML na serikali imezingatia mfumo shirikishi sambamba na sheria za aridhi ili kutoa fidia stahiki.

Gombati amesema waathirika wa mtaa wa Nyakabale ni watu wapatao 4,665 katika eneo lenye ukubwa wa hekta 4,940 ambao hatua zinafanyika kuwapatia eneo mbadala na salama la makazi.

Amesema eneo ambalo limependekezwa ni hekta 1,000 kutoka hifadhi ya msitu wa Geita ambapo iwapo Wizara ya Maliasili na Utalii itaridhia viwanja kupimwa na eneo litafanyiwa mpango mji.

“Eneo la hifadhi ya msitu wa Geita lina ukubwa wa hekta 54,000 ambapo zikitolewa hekta 1,000 tutasalia na hekta 53,000,” amesema Gombati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *