Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) limeunga mkono haki ya Wapalestina ya kujiainishia hatima na mustakabali wao.

Kulingana na Pars Today, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa wingi wa kura azimio linalothibitisha haki ya watu wa Palestina ya kujiamulia mambo yao, ikiwa ni pamoja na haki ya kuwa na taifa huru la Palestina. Azimio hilo lilipitishwa kwa kuungwa mkono na nchi wanachama 164, huku kura nane pekee zikilipinga. Aidha nchi tisa pia zilijizuia kupiga kura.

Azimio hilo, lenye anuani isemayo: “Haki ya Watu Kufanya Maamuzi,” limethibitisha tena msimamo wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya Wapalestina kuamua kwa uhuru hadhi yao ya kisiasa na kufuata maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Azimio hilo liliashiria maazimio na vyombo husika vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, na kuthibitisha kwamba haki ya kujiamulia hatima na mustakabai ni kanuni ya msingi ya sheria ya kimataifa. Azimio hilo pia liliyataka mataifa yote, mashirika na asasi za Umoja wa Mataifa kuwaunga mkono na kuwasaidia Wapalestina katika utekelezaji wa haraka wa haki hii.

Zaidi ya hayo, azimio hilo lilisisitiza hitajio la kuheshimu umoja wa ardhi wa eneo la Palestina iliyokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Baytul-Muqaddas Mashariki, na kusisitiza tena kuunga mkono amani na haki ya kudumu na ya kina inayotegemea sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Kupasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa haki ya Wapalestina ya kujiamulia mambo yao ni mojawapo ya uthibitisho muhimu zaidi wa kimataifa wa haki za mataifa. Uamuzi huu hautegemei tu kanuni za msingi za sheria za kimataifa, bali pia unaakisi mapambano ya miongo kadhaa ya watu wa Palestina ili kupata uhuru na kukomesha uvamizi huo.

Ili kuelewa sababu za hatua hii na matokeo yake, ni muhimu kuzingatia mihimili kadhaa ya msingi.

Kwanza, kanuni ya haki ya kujitawala ni mojawapo ya kanuni za msingi za mkataba wa Umoja wa Mataifa. Kanuni hii inasema kwamba, watu wote wana haki ya kuamua kwa uhuru hali yao ya kisiasa na kuchagua njia ya maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Kwa upande wa Palestina, haki hii imesisitizwa mara kwa mara katika hati za kimataifa. Tangu Azimio la Baraza la Usalama nambari 242 baada ya vita vya 1967 hadi maazimio mengi ya Baraza Kuu, umuhimu wa kukomesha uvamizi wa maeneo ya Palestina na kutambua taifa huru la Palestina umekuwa ukisisitizwa kila wakati. Kwa hivyo, uamuzi wa hivi karibuni wa Baraza Kuu ni muendelezo wa njia hiyo hiyo ya kisheria na kisiasa.

Pili, kuna haja ya kutoa uzingatiaji maalumu kwa kadhia ya Palestina katika mfumo wa kimataifa. Watu wa Palestina wameishi kwa miongo kadhaa chini ya uvamizi wa kijeshi na vikwazo vikali. Ujenzi mkubwa wa vitongoji vya walowezi, mzingiro dhidi ya Gaza, sheria kali za kutembea, na ukiukwaji wa haki za binadamu vyote vimeunda mazingira ambayo jamii ya kimataifa haiwezi kubaki bila kujali. Kuthibitisha haki ya Wapalestina ya kujitawala kwa kweli ni jibu kwa hali hii na jaribio la kurejesha haki kwa watu ambao wamenyimwa haki zao za msingi.

Maandamano ya kuunga mkono Palestina

Tatu ni shinikizo la maoni ya umma duniani na jukumu la nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Serikali nyingi, hasa katika nchi za Kusini na Kiislamu duniani, zimeunga mkono kadhia ya Palestina kwa miaka mingi. Uungaji mkono huu umeonekana katika Baraza Kuu na umepelekea kupitishwa kwa maazimio yanayotambua haki ya Wapalestina ya kujiamulia mambo yao. Hapana shaka kuwa, uamuzi huu ni matokeo ya makubaliano mapana ambayo yanavuka mipaka ya kisiasa na kiitikadi na yanategemea kanuni za kibinadamu na haki.

Alaa kulli haal, kuunga mkono Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa haki ya kujitawala kwa Wapalestina kuna umuhimu mkubwa wa kisheria na kisiasa. Hatua hii sio tu kwamba inazingatia misingi ya haki na haki za binadamu, lakini pia inatoa ujumbe wa wazi kwa ulimwengu kwamba, uvamizi na unyimwaji wa haki za kimsingi hauwezi kuendelea milele.

Ingawa njia ya utekelezaji wa haki hii kivitendo bado ni ngumu na yenye changamoto, lakini uungaji mkono huu ni hatua muhimu katika njia ya kufikia uadilifu wa kihistoria kwa watu wa Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *