
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Mpango wa Elimu kwa Umma Kuhusu Muungano utakuwa endelevu ili kuhakikisha elimu hiyo inamfikia kila mmoja.
Ameyasema hayo leo Desemba 19, 2025 wakati akizungumza katika kipindi cha Asubuhi Njema kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Amesema Waandishi wa Habari wana nafasi kubwa katika utoaji wa elimu kwa umma ndio maana Ofisi ya Makamu wa Rais imewapa nafasi na itakuwa ikishirikiana nao kwa asilimia kubwa.

“Katika kuhakikisha hilo leo tumeandaa Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari Zanzibar kisha tutaifanya kwa Wahariri Bara na baadaye tutaandaa makongamano mbalimbali,” amesema Mhandisi Masauni.
Amesema wanufaika wakubwa wa Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Muungano, watakuwa vijana ambao ndio walengwa kutokana na wengi wao kuwa wamezaliwa baada ya Muungano (1964).