Vikosi vya usalama vya Tanzania vilitumia nguvu kubwa kupita kiasi, ikiwemo mauaji, katika kuzima maandamano ya uchaguzi yaliyofanyika kati ya tarehe 29 Oktoba na 3 Novemba 2025, kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la haki za binadamu la Amnesty International. Ripoti hiyo inaeleza kuwa hatua hizo zilionesha kiwango cha kutisha cha kutojali haki ya uhai na uhuru wa kukusanyika kwa amani.
Kwa mujibu wa Amnesty International, mamia ya watu wanadaiwa kuuawa au kujeruhiwa wakati wa operesheni za vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Shirika hilo linasema matumizi ya nguvu hayakuwa ya uwiano na yalikiuka viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Katika kukusanya taarifa zake, Amnesty International ilifanya mahojiano na watu 35, wakiwemo manusura wa kupigwa risasi, waliopata majeraha kutokana na mabomu ya machozi, mashuhuda wa matukio, mawakili waliowatetea waandamanaji waliokamatwa, wahudumu wa afya waliowahudumia majeruhi, pamoja na ndugu wa watu waliouawa.
Mahojiano hayo yalifanyika kati ya tarehe 3 na 28 Novemba 2025, yakilenga kupata ushahidi wa moja kwa moja kuhusu matumizi ya nguvu na athari zake kwa raia waliokuwa wakishiriki maandamano ya kisiasa baada ya uchaguzi.
Uthibitishaji wa video na picha za matukio
Kupitia kikundi chake cha uchunguzi wa kidijitali kinachojulikana kama Maabara ya Ushahidi, Amnesty International ilithibitisha video 26 na picha sita zilizokuwa zikisambazwa mtandaoni au kutumwa moja kwa moja kwa wafanyakazi wa shirika hilo na vyanzo vya kuaminika.
Mtafiti wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki, Sikula Oniala, anasema uchambuzi wa nyenzo hizo unaonesha wazi matumizi ya nguvu zisizo na uwiano, ikiwemo matumizi ya risasi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha.
Oniala anasema kuwa ushahidi uliokusanywa unaashiria mauaji makubwa yaliyotekelezwa na vikosi vya usalama katika jitihada za kuzima maandamano, hali ambayo ilisababisha vifo vya watu wengi katika maeneo tofauti ya nchi.
Maabara ya Ushahidi ilithibitisha video moja inayoonesha takribani maiti 70 zikiwa zimerundikwa sakafuni na kwenye machela katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Aidha, video mbili na picha moja zilithibitishwa zikionesha takribani maiti 10 zikiwa zimerundikwa kwenye machela tatu nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure jijini Mwanza, jambo lililoongeza maswali kuhusu idadi halisi ya waliopoteza maisha.
Baadhi ya wananchi wamesema ripoti hiyo imeibua upya mjadala kuhusu kile kilichotokea wakati wa maandamano. Mkazi wa Dar es Salaam, Erard Mporoto, anasema ripoti hiyo inatoa msingi kwa umma kutarajia uwajibikaji na ufafanuzi zaidi.
Je, Serikali Ilishirikishwa?
Kwa mujibu wa Amnesty International, shirika hilo liliwasiliana na serikali ya Tanzania kuomba maoni yake kabla ya kuchapisha ripoti hiyo, lakini hadi wakati wa kutolewa kwa taarifa hiyo, halikuwa limepokea majibu yoyote rasmi.
Shirika hilo linasisitiza kuwa mamlaka za Tanzania zinapaswa kuhakikisha kuwa uchunguzi wowote kuhusu matukio hayo unakuwa huru, wa kina na usio na upendeleo, ili haki ipatikane kwa waathirika na familia zao.
Amnesty International iliwahoji wanafamilia na marafiki wa watu wanane waliouawa katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tunduma, Moshi na Mbeya, ambao walisema hawakuweza kupata miili ya wapendwa wao.
Baadhi ya familia hizo zina hofu kwamba vikosi vya usalama vilichukua miili ya waliouawa kwa lengo la kuficha ushahidi wa mauaji, jambo linaloongeza maumivu na maswali yasiyopata majibu.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Gwandumi Mwakatobe, anasema ripoti hiyo inaakisi kile ambacho wananchi wengi walikishuhudia mitaani, akidai kuwa vyombo vya usalama vilionekana kubadilika na kuwa vyombo vya ukatili dhidi ya raia.
Ripoti hii inajitokeza katika mazingira ya uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 98 ya kura, matokeo yaliyofuatiwa na maandamano katika baadhi ya maeneo nchini.
